Madrid, Hispania
Baada ya Rais wa Shirikisho la Soka Hispania (REEF), Luis Rubiales kukataa kujiuzulu kwa kosa la kumpiga busu mdomoni mshambuliaji wa timu ya taifa ya wanawake, Jenni Hermoso, wachezaji 81 wanawake wa Hispania wametangaza kugoma kuichezea timu ya taifa.
Katika taarifa yake hata hivyo REEF imeonya ikidai kwamba mchezaji yeyote anayechaguliwa kuiwakilisha timu ya taifa ana wajibu wa kufanya hivyo.
Mbali na Hispania, sakata la Rubiales limeanza kusambaa katika nchi nyingine likihusisha zaidi wanawake ambapo Jumamosi nchini Marekani katika mechi ya ligi ya wanawake kati ya Orlando Pride and San Diego Wave kulikuwa na matukio ya kumtetea Jenni na kadhia iliyomkuta.
Katika mechi hiyo wachezaji walivaa beji maalum za kumuunga mkono Jenni, beji hizo zilikuwa na maandishi yaliyosomeka ‘Contigo Jenni’ yaani tuko pamoja nawe Jenni.
Mmoja wa wachezaji wa Marekani aliye mstari wa mbele ni mshambuliaji Alex Morgan ambaye kabla ya hapo alinukuliwa akisema, “Nimeshtushwa na msimamo wa watu kwa alichokifanya Luis Rubiales, niko pamoja na Jenni Hermoso na wachezaji wa Hispania.
“Kushinda Kombe la Dunia inatakiwa liwe tukio bora na la kipekee katika maisha ya wachezaji hawa badala yake linafunikwa na udhalilishaji, uhuni na kushindwa kwa shirikisho la soka Hispania.
England nako timu ya wanawake ambayo ilipoteza katika mechi ya fainali ya Kombe la Dunia la Wanawake (WWC) dhidi ya Hispania kwa kufungwa bao 1-0, taarifa yao imesema kwamba alichofanya Rubiales hakikubaliki.
“Tabia za watu wanaodhani kwamba wao ni imara na hawaadhibiwi, watu hawa wasivumiliwe, watu wasichukulie namna nyingine mambo wanayoyafanya ya aina yoyote ya udhalilishaji. Jenni Hermosso tunasimama pamoja nawe,” ilieleza taarifa ya timu ya wanawake ya England.
Jumapili iliyopita, Rubiales alimpiga busu la mdomoni, Jenni mara baada ya Hispania kuichapa England bao 1-0 katika mechi ya fainali dhidi ya England, kitendo hicho ambacho alikifanya wakati wachezaji wakipewa medali, kimetafsiriwa kuwa ni udhalilishaji kwa wanawake kwani mchezaji huyo hakufanyiwa jambo hilo kwa ridhaa yake.
Kombe la Dunia Wachezaji timu ya taifa Hispania wagoma
Wachezaji timu ya taifa Hispania wagoma
Read also