Na mwandishi wetu
Mchuano ya wazi ya mchezo wa gofu ya kimataifa yaliyopewa jina la NCBA Golf Open inatarajia kufanyika Novemba 23 hadi 26, mwaka huu mkoani Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam Jumatano hii kwenye utambulisho wa mdhamini wa shindano hilo, Mwenyekiti wa Chama cha Gofu Tanzania (TGU) Gilman Kasiga alisema shindano hilo linatarajiwa kushirikisha zaidi ya wachezaji 200 kutoka nchi za Afrika.
“Kwanza natoa shukrani zangu za dhati kwa benki ya NCBA kwa ushirikiano mliotuonesha kama mfadhili mkuu wa mashindano, ahadi yenu ya kukuza gofu nchini ni ya kupongezwa kwani michuano hii pia itahusisha wachezaji maarufu wa nchi za Kenya, Uganda, Rwanda, Afrika Kusini, Ethiopia na Zimbabwe,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NCBA, Claver Serumaga alisema ana furaha kwa ushirikiano huo unaowaunganisha na wacheza gofu akisema wamelenga kuinua mchezo huo kuanzia chini.
“Tunajivunia kutangaza ushirikiano huu na TGU, mashindano haya yanaonesha ahadi yetu thabiti katika mchezo wa gofu na kujitolea kwetu kuinua vipaji bora Afrika Mashariki ili kushindana na kuonesha ujuzi wao,” alisema Serumaga.
Nao Vodacom ambao ni wadhamini pia wa michuano hiyo, kupitia kwa meneja wake mkuu wa Masoko, Ailen Meena alisema wamekuwa wakijihusisha kusaidia michezo mbalimbali na awamu hii wanashirikiana na TGU kufanikisha maandalizi ya mashindano hayo na kuhimiza wadau wengine wajitokeze kuungana nao kulifanya shindano kuwa zuri.