Na mwandishi wetu
Kaimu kocha mkuu wa Taifa Stars, Hemed Suleiman ‘Morocco’ amesema Dickson Job hakuwa mzalendo kwa kukataa kucheza eneo alilompangia.
Hivi karibuni, Morocco aliita kikosi cha wachezaji 23 ambao watakwenda Azerbaijan kwenye michezo ya Fifa Series 2024 huku akiwaacha nyota kadhaa waliocheza Afcon nchini Ivory Coast hivi karibuni akiwemo Job hali iliyoibua maswali kwa mashabiki.
Akitolea ufafanuzi suala hilo leo Ijumaa, Morocco alisema wanaozungumzia suala hilo hawamsaidii Job ila wanapaswa kuheshimu maamuzi ya kocha kwani walizungumza yakaisha salama lakini wakiendelea kuzungumza watamvunja moyo.
“Mimi namlinda, ni mchezaji mzuri na anastahili kucheza timu ya taifa, watu wangeliacha hili kama lilivyo maana nikilitolea ufafanuzi mimi nitakua ‘namuua’, ni kweli alifanya makosa nimempumzisha kulingana na mahitaji ya mechi tunayokwenda kucheza na ana nafasi kwa wakati mwingine,” alisema Morocco.
Job alikataa kucheza mechi dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia Congo (DRC) ambapo Morocco alimpanga kucheza beki wa kulia katika mechi iliyomalizika kwa suluhu.
Morocco anasema Job alipogundua kosa alirudi kuomba msamaha, alipoulizwa kama angeweza kucheza alipoumia Lusajo Mwaikenda akajibu ndiyo, akaulizwa sasa kwa nini alikataa kucheza akakosa jibu.
Mara kadhaa Job amekuwa akicheza Yanga kama beki wa kati huku wakati mwingine akitumika kama beki wa pembeni anapokuwa na Stars kama vile ilivyokuwa wakati Stars inashinda bao 1-0 dhidi ya Uganda nchini Misri hivi karibuni na ni Job ndiye aliyepiga krosi iliyozaa bao hilo lililofungwa na Simon Msuva.
Mara kadhaa wakati wa kocha Nasreddine Nabi akiwa Yanga, Job alishuhudiwa akicheza pembeni, hivyo kukataa kwake kuitumikia nafasi hiyo akiwa na Stars ilionekana kama kukosa uzalendo kwa nchi ikiwa vitani japo Morocco anasema wameyazungumza na yamekwisha.