Abidjan, Ivory Coast
Mshambuliaji wa zamani wa Chelsea, Didier Drogba amesema kwamba wanasoka wa Afrika wanatakiwa kuwa makini na mawakala feki wanaowapa ahadi za kupata utajiri na kuwa maarufu.
Droga ametoa kauli hiyo kupitia taasisi yake ambayo inashirikiana na Umoja wa Wanasoka Duniani (FIFPRO) na Shirika la Kazi la Umoja wa Mataifa (ILO) ili kuwahamasisha wanasoka kuhusu hatari hiyo.
“Tafadhali ningependa msikilize jambo hili, kuweni makini kuhusu nani wa kumuamini, katu usimuamini mtu anayetaka fedha zako,” alisema Drogba ambaye pia amewahi kuwa mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Ivory Coast.
FIFPRO hivi karibuni ilifanya utafiti kwa wanasoka 263 kutoka nchi saba za Afrika na kubaini asilimia 70 ya wanasoka hao waliwasiliana na watu ambao waliwapa ahadi ya kuwasaidia kuhamia klabu fulani.
Katika utafiti huo asilimia 43 ya wanasoka wanaofuatwa hupewa nafasi ya kwenda kufanya majaribio au mikataba na klabu na asilimia 56 hawapati ahadi waliyopewa ya kwenda kufanya majaribio na asilimia 44 hawasaini mikataba wanayotarajia kusaini.
“FIFPRO imesikia habari nyingi za wachezaji wanaofuatwa na watu wanaojifanya mawakala na kuwapa ahadi ya kuwatafutia timu za kufanya majaribio au mikataba na klabu mpya,” ilieleza taarifa ya FIFPRO.
“Ukweli huwa ni tofauti, katika matukio mabaya zaidi wanasoka hujikuta wamekwama katika nchi za watu wakiwa hawana fedha za kurudi nyumbani.”
Drogba alisema kwamba wachezaji chipukizi ndio hasa walio katika hali ya hatari kutokana na shauku yao ya kumpata wakala.
“Wakala mzuri si mtu ambaye unaweza kumuamini, wakala mzuri unayeweza kuwa naye ni uchezaji wako bora wa soka, hili huwa haliongopi, kwa hiyo unapocheza vizuri ndipo klabu nyingi zinapokufuata kukuangalia unavyocheza,” alisema Drogba.
“Ninachokiona ni kwamba kuna watoto wengi wanaohaha kumkimbilia wakala wa kuwatafutia klabu, mambo hayaendi hivyo, ni kiwango chako ndicho kitakachozivutia klabu pamoja na mawakala walio wazuri,” alisema Drogba.
“Baadhi ya marafiki zetu wanalipa akiba ya familia yao yote, kila walichonacho lakini hawaendi kucheza kokote wanaishia kuachwa wakitangatanga kwenye uwanja wa ndege au maeneo ya hovyo na wengine hata kuishia jela katika nchi za Asia,” aliongeza Drogba.
Kwa mujibu wa sheria mpya za Fifa kila wakala wa soka ni lazima awe na leseni ya Fifa ambayo itamtaka kwanza awe amefaulu mtihani.
