Milan, Italia
Mshambuliaji wa AC Milan, Zlatan Ibrahimovic amewashutumu wachezaji wa timu ya Argentina kwa namna walivyokuwa wakiwadhihaki wenzao wa Ufaransa baada ya kulibeba Kombe la Dunia.
Desemba 18 mwaka jana, Argentina ilifanikiwa kubeba Kombe la Dunia baada ya kuibwaga Ufaransa kwa penalti 4-2 katika mechi ya fainali iliyochezwa kwa dakika 120 na kumalizika kwa sare ya 3-3.
Baada ya ushindi huo na kuifanya nchi hiyo kubeba kwa mara ya kwanza taji hilo tangu mwaka 1986, baadhi ya wachezaji wa Argentina walirekodiwa wakimdhihaki mchezaji nyota wa Ufaransa Kylian Mbappe kwenye vyumba vya kubadilishia nguo huku kipa Emilio Martinez akiendeleza dhihaka hizo dhidi ya Mbappe wakati akiwa kwenye basi la wazi na wachezaji wenzake.
Akizungumza jana Jumatano, Ibrahimovic ambaye anatokea nchini Sweden, alisema kwamba wachezaji hao walionyesha tabia mbaya na hawatokumbukwa kwa lolote zaidi ya nahodha wao, Lionel Messi.
“Messi anatajwa kuwa mchezaji bora katika historia ya soka, nilikuwa na uhakika alikuwa anakwenda kushinda Kombe la Dunia, kitakachotokea tena ni kwamba na Mbappe atashinda taji hilo,” alisema.
“Sina hofu kuhusu Mbappe, hofu yangu ni kwa wachezaji wengine wa Argentina kwani hawatoweza kushinda zaidi ya hilo, Messi ameshashinda kila kitu na atakumbukwa lakini wengine watakumbukwa kwa namna walivyoonyesha tabia mbaya, hatuwezi kuheshimu hilo,” alisema Ibrahimovic.
“Hili linatoka kwangu, ni kauli ya mchezaji profesheno wa kiwango cha juu, mlichofanya (Argentina) ni ishara kwamba mtashinda mara moja, hamtoshinda tena, huwezi kushinda kwa namna hiyo,” aliongeza mshambuliaji huyo aliyewahi pia kuchezea timu mbalimbali kubwa barani Ulaya.
Naye kiungo wa zamani wa timu ya Taifa ya Ufaransa, Patrick Vieira alisema alisikitishwa kwa namna Martinez alivyoshangilia kwa dhihaka baada ya Argentina kubeba Kombe la Dunia kwa kuwabwaga Ufaransa waliokuwa mabingwa watetezi.