Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Simba, Abdelhak Benchikha amewataka wachezaji wake kusahau ushindi wa mabao 6-0 walioupata dhidi ya Jwaneng Galaxy na kufuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Badala yake kocha huyo amewataka wachezaji hao kuhamishia akili na nguvu zao katika kuzisaka pointi 12 za michezo minne ijayo ya Ligi Kuu NBC.
Simba inakabiliwa na michezo minne inayotarajiwa kupigwa Machi 6, 9, 12 na 15, huku michezo mitatu wakicheza kwenye Uwanja wa wa Jamhuri, Morogoro na mmoja ukipigwa ugenini Mkwakwani, Tanga.
Wekundu hao kesho watashuka uwanjani kuikabili Tanzania Prisons, kisha watasafiri kuikabili Coastal Union na baadaye watarejea nyumbani kumenyana na Singida Fountain Gate FC kabla ya kumalizana na Mashujaa FC.
“Tuna ratiba ngumu mbele yetu lakini tumefanikiwa kuvuna pointi na kuonesha ubora katika michezo iliyopita, bado tuna kazi ya kufanya na sasa tunapaswa kuonesha ukubwa wetu kwenye mechi zinazofuata.
“Tumecheza vizuri sana katika michezo ya nyuma, ubora wa mechi ile (6-0) uliooneshwa na wachezaji wangu nina imani utaendelea kuonekana katika mechi zijazo na kuitumia michezo hiyo kama sehemu ya maandalizi ya mechi za robo fainali,” alisema Benchikha.