Naples, Italia
England imeilaza Italia mabao 2-1 ikiwa ni ushindi wao wa kwanza ugenini dhidi ya timu hiyo tangu mwaka 1961 huku nahodha Harry Kane akiweka rekodi ya kuwa mfungaji wa timu hiyo mwenye mabao mengi.
Katika mechi hiyo ya kuwania kufuzu Euro 2024 iliyopigwa jana Alhamisi mjini Naples, Kane aliweka rekodi hiyo katika dakika ya 44 kwa bao la penalti na kuwa bao lake la 54 kuifungia England.
Kwa bao hilo, Kane sasa anakuwa amempiku mshambuliaji wa zamani wa timu hiyo, Wayne Rooney ambaye kwa muda mrefu alikuwa akishikilia rekodi ya kuifungia England mabao mengi.
Declan Rice ndiye aliyefunga bao la kwanza la England katika dakika ya 13 akimalizia shuti la Kane ambalo awali liliokolewa.
Bao pekee la Italia lilifungwa na Mateo Retegui katika dakika ya 56 akineemeka na makosa yaliyofanywa na beki wa England, Harry Maguire kuchelewa kuokoa mpira.
Zikiwa zimebaki dakika 10 mpira kumalizika, England ilipata pigo baada ya Luke Shaw kulimwa kadi ya pili ya njano na hivyo kuiacha timu hiyo na wachezaji 10 uwanjani lakini ilifanikiwa kulinda ushindi.
Shaw alipewa kadi ya kwanza ya njano dakika ya 78 kwa kuchelewa kurusha mpira wakati kadi ya pili iliyomfanya atoke uwanjani alipewa dakika mbili baadaye kwa kumchezea rafu mfungaji wa bao la Italia, Retegui.
Baada ya ushindi huo dhidi ya timu inayotajwa kuwa ngumu katika kundi lake, England sasa itakuwa na kazi ya kujiweka vizuri ili kuhakikisha inafuzu Euro 2024 keshokutwa Jumapili itakapoumana na Ukraine kwenye dimba la Wembley. Timu nyingine zilizo kundi moja na England ni Malta na North Macedonia.
Matokeo ya mechi nyingine za kufuzu Euro 2024 zilizochezwa jana Alhamisi ni kama ifuatavyo…
Portugal 4-0 Liechtenstein
Italia 1-2 England
San Marino 0-2 N. Ireland
Kazakhstan 1-2 Slovenia
Bos-Herze 3-0 Iceland
Slovakia 0-0 Luxembourg
North Macedonia 2-1 Malta
Denmark 3-1 Finland
Kimataifa Kane aweka rekodi England
Kane aweka rekodi England
Read also