Na mwandishi wetu
Mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya NBC, Yanga imeweka wazi kuwa kambi yake ya kujiandaa na msimu ujao itakuwa Avic Town, Kigamboni na si tena Morogoro wala nje ya nchi kama ilivyokuwa ikielezwa hapo awali.
Awali ilielezwa kuwa Yanga inaweza kwenda kuweka kambi nchini Uturuki lakini baadaye ikaahirishwa ikielezwa kuwa muda hauwatoshi kulingana na ratiba ya msimu ujao hivyo wangeenda Morogoro, kabla ya leo kutangaza mpango mpya na rasmi.
Ofisa Habari wa Yanga, Haji Manara ameeleza hayo leo ikiwa ni pamoja na kutangaza rasmi juu ya kuachana rasmi na mshambuliaji Chico Ushindi raia wa DR Congo na mazungumzo waliyonayo juu ya kumalizana na straika wao, Yacouba Sogne kutoka Burkin Fasso.
Akizungumzia suala la kambi, Manara alisema kambi hiyo itaanza rasmi Ijumaa hii na moja kwa moja wataingia kambini, hiyo ni kutokana na ombi la benchi la ufundi likitaka kurefushwa kwa siku za mapumziko za wachezaji kutokana na kazi nzito waliyoifanya msimu uliomalizika hivi karibuni.
“Kambi yetu ya maandalizi msimu ujao itakuwa Avic Town, na wachezaji wataanza kurudi kesho tarehe 20 na moja kwa moja wataingia kambini.
“Tulipanga likizo yetu kumalizika Julai 15, lakini makocha wakashauri tuwaongezee wachezaji wetu muda wa mapumziko kwa sababu walikuwa na msimu mrefu na hawakupata nafasi ya kupumzika kutokana na majukumu ya klabu na timu za Taifa,” alisema Manara.
Kuhusu kitendawili cha kuwa na wachezaji 14 wa mataifa ya nje 14 badala ya 12 kama kanuni za ligi zinavyosema, Manara ameeleza hilo limeshashughulikiwa na kuwataja watakaopunguzwa kuwa ni Chico na Sogne.
“Mnaweza kujiuliza vipi mnaingia ‘pre-season’ na wachezaji 14, lakini tumekubaliana na mchezaji wetu ambaye tumekuwa naye tangu dirisha dogo mpaka sasa tuliyemchukua kwa makubaliano maalum baina yetu na Mazembe, Chicho Ushindi tumekubaliana baada ya mapendekezo na walimu tumrudishe Mazembe akaendelee kucheza kule kwa hiyo hatutakuwa naye msimu ujao.
“Pia Yacouba bado hajawa fiti asilimia mia moja kwa mujibu wa ripoti za kitabibu na tutamwita sehemu ya wachezaji, tutakaa naye chini kuona tunaweza kufanyaje baina ya Yanga na Yacouba katika kipindi hiki ambacho anahitaji zaidi ‘recovery’ kuliko kuanza kutumika moja kwa moja,” alisema Manara.
Pamoja na hayo, Manara aligusia kuhusu ratiba yao ya Wiki ya Wananchi ambapo safari hii itaanza Agosti Mosi, kilele chake kikitarajiwa kuwa Agosti 6, mwaka huu akieleza timu watakayocheza nayo itakuwa timu ya kiwango chao kwa kuwa nao ni mabingwa kama wao. Mwisho akadokeza kuwa wiki ijayo kama mambo yatakwenda kama yalivyopangwa watazindua jezi zao mpya watakazotumia msimu mpya wa 2022/23.
Soka Kambi Yanga ni Kigamboni
Kambi Yanga ni Kigamboni
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
