Na mwandishi wetu
Kipa namba moja wa Yanga aliyekuwa majeruhi, Djigui Diara anatarajia kuwamo katika kikosi cha Yanga kitakachoumana na TP Mazembe katika mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Diarra aliyekuwa majeruhi akisumbuliwa na misuli alilazimika kutolewa katika mechi ya awali ya Yanga dhidi ya Mazembe iliyopigwa Desemba 14, 2024 mjini Lubumbashi DR Congo.
Katika mechi hiyo iliyoisha kwa sare ya bao 1-1, Diarra alishindwa kuendelea na mechi kipindi cha pili na nafasi yake kuchukuliwa na Aboubakar Khomeiny.
Kuumia huko kulimpa nafasi Khomeiny kucheza mechi hiyo na nyingine za Ligi Kuu NBC lakini hivi karibuni Yanga imekuwa ikimtumia kipa wake mwingine wa akiba, Abutwalib Mshery.
Kurejea kwa Diarra ni habari pendwa kwa baadhi ya mashabiki wa Yanga ambao walikuwa na wasiwasi na makipa wao wa akiba kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa Afrika ambazo timu yao haina matokeo mazuri.
Katika ligi hiyo, Yanga imeshacheza mechi tatu ikilala kwa mabao 2-0 mbele ya Al Hilal ya Sudan jijini Dar es Salaam kabla ya kuchapwa mabao kama hayo na MC Alger ugenini Algeria.
Kwa matokeo hayo Yanga iliyo Kundi A hadi sasa ina pointi moja tu na ndiyo inayoburuza mkia katika kundi hilo hivyo mechi dhidi ya Mazembe itakayopigwa Januari 4, 2025 huenda ikawa fursa ya timu hiyo kurejesha matumaini ya kufuzu hatua ya robo fainali.
Kimataifa Diarra kuivaa Mazembe Dar
Diarra kuivaa Mazembe Dar
Read also
