Na mwandishi wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene ameiomba klabu ya Simba kama imebaini vitendo vya rushwa katika mchezo wake na Yanga kutoa taarifa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Manispaa ya Temeke kwa hatua zaidi.
Hiyo ni baada ya Simba kudaiwa kuwasimamisha baadhi ya wachezaji kwa uchunguzi juu ya tuhumu za kupokea rushwa walipofungwa mabao 5-1 na Yanga Jumapili iliyopita kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
Simbachawene (pichani) amezungumza hayo bungeni jijini Dodoma leo Jumatano wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Makete, Festo Sanga aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kupambana na rushwa michezoni.
Mbunge huyo katika hoja yake alitolea mfano baadhi ya wachezaji wa Simba kusimamishwa kwa madai ya kuwepo kwa viashiria vya rushwa katika mchezo huo.
“Rushwa michezoni haikubaliki kama mchezo wa juzi wa Yanga na Simba una viashiria vyovyote vya rushwa, niwaombe sana Simba kama zile tano zimetokana na rushwa waende Takukuru Temeke ili hatua zichukuliwe,” alisema Simbachawene.
Awali, akijibu swali hilo Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Hamis Mwinjuma ‘MwanaFA’ alisema wizara hiyo kwa kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imekua ikipinga vitendo vya rushwa michezoni.
Alisema kwa kushirikiana na Takukuru wamekua wakitoa elimu kuhusu suala hilo na kwamba tayari wameanzisha kampeni ya ‘Kataa upangaji wa matokeo, linda hadhi ya mpira wa miguu’ ambayo inaendelea kuleta matokeo mazuri.
Alisema kuwa wadau wengine wa michezo kama klabu wamekuwa wakishiriki kupinga vitendo hivyo.