Na mwandishi wetu
Namungo wameifuata Yanga kwa tahadhari wakisema wanajua aina ya mpinzani wanayekwenda kucheza naye hivyo wamejipanga kwa mapambano.
Yanga itakuwa mwenyeji wa Namungo katika mchezo wa Ligi Kuu NBC utakaochezwa keshokutwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.
Akizungumza na GreenSports, Kocha Mkuu wa Namungo, Denis Kitambi alisema wanatarajia kutua Dar es Salaam leo Alhamisi wakitokea Ruangwa mkoani Lindi na kesho watafanya mazoezi ya mwisho kujiweka imara kwa ajili ya mchezo huo.
“Tumefanya maandalizi mazuri dhidi ya Yanga na tunajua tunakwenda kucheza na timu inayoongoza ligi lakini pia, idara yao ya ulinzi hairuhusu mabao, wako vizuri hivyo tunapaswa kucheza kwa tahadhari lakini tumejipanga dhidi yao na lengo letu ni kupata pointi tatu,” alisema.
Kitambi alisema wanawaheshimu wapinzani wao wakiamini mchezo hautakuwa mwepesi kwa kuwa kila mmoja anataka pointi tatu ili kuwa katika nafasi nzuri.
Yanga ndiye kinara wa ligi anayeongoza kwa pointi 56 katika michezo 21 huku Namungo ikishika nafasi ya sita kwa pointi 29.
Soka Namungo yajipanga kimapambano
Namungo yajipanga kimapambano
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
