Na mwandishi wetu
Timu ya Ihefu imetangaza usajili wa wachezaji wawili, beki David Mwantika (pichani juu) na mshambuliaji Adam Adam kwa ajili ya kuhakikisha wanaiimarisha timu hiyo kuelekea mechi za lala salama za Ligi Kuu NBC.
Usajili huo uliotangazwa jana ndiyo wa kwanza kwa timu hiyo tangu kufunguliwa kwa dirisha dogo la usajili msimu huu Desemba 16 mwaka jana likitarajiwa kufungwa Januari 15, mwaka huu.
Akizungumza na GreenSports, kocha msaidizi wa Ihefu, Zuberi Katwila alisema usajili huo umekuwa na mantiki kwao kwani ni nafasi muhimu wameongeza kwenye timu hasa ukizingatia ni wachezaji mahiri wenye uozefu na ligi.
“Tumeongeza nafasi ambazo tulikuwa tunahitaji zaidi kuongeza, ni mahitaji ambayo yanahitajika na kwa wachezaji waliokuja wataleta ushindani kwenye safu zao wakisaidiana na waliowakuta kuhakikisha tunamaliza vizuri ligi,” alisema Katwila.

Mwantika aliyewahi kukipiga Azam na kisha kuisaidia Singida Big Stars kupanda Ligi Kuu msimu huu ametua katika kikosi hicho kama mchezaji huru huku Adam (pichani katikati) akitua hapo akitokea Mtibwa Sugar.
Ihefu ambayo haina matokeo mazuri tangu kuanza kwa msimu, inashikilia nafasi ya 13 ikiwa na pointi 20 baada ya michezo 19.
