Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Ihefu FC, Mecky Maxime amesema matokeo ya sare ya kufunga bao 1-1 dhidi ya Mashujaa FC yamevuruga hesabu zao za kupanda nafasi za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC.
Maxime alisema mchezo huo uliopigwa Uwanja wa Liti, Singida ulikuwa mgumu na kila timu ilipambana kutafuta ushindi lakini kujisahau kwa mabeki wake kuliwanufaisha wapinzani wao na kusawazisha bao hilo la mapema dakika ya 11 lililofungwa na Elvis Rupia.
“Sijafurahishwa na matokeo haya lakini hatuwezi kukata tamaa bado tuna mechi nyingi za kucheza nyumbani na ugenini, naamini tutapata matokeo mazuri yatakayotupandisha nafasi za juu,” alisema Maxime nahodha wa zamani wa Taifa Stars.
Naye kocha mkuu wa Mashujaa, Abdallah Mohamed ‘Baresi’ alisema wakati wanaingia uwanjani kuikabili Ihefu walijua utakuwa mchezo mgumu hivyo walijipanga kuhakikisha wanapata ushindi au sare na anashukuru Mungu, moja ya malengo yao kufanikiwa.
“Ulikuwa mchezo muhimu kwetu sote Ihefu na sisi Mashujaa lakini tunashukuru kwa hiki kidogo tulichokipata, naamini itakuwa na maana kubwa kwetu katika harakati zetu za kujiondoa nafasi ya chini tuliyopo,” alisema Baresi.
Ihefu ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC ikikusanya pointi 20 katika mechi 18 wakati Mtibwa imebaki nafasi ya 15 wakiwa na idadi kama hiyo ya pointi.