Doha, Qatar
Kocha wa Ufaransa, Didier Deschamps amesema kwamba hawasumbuliwi na mtazamo wa ‘watu wengi’ kutaka nyota wa Argentina, Lionel Messi abebe taji la dunia wakati timu hizo zitakapokutana katika fainali Jumapili hii.
Deschamps leo anawania kuweka rekodi ya kubeba taji la dunia mara ya pili mfululizo huku kukiwa na mtazamo wa wengi kwamba safari hii Messi ataweka rekodi kwa kubeba kwa mara ya kwanza taji hilo akiwa na jezi ya Argentina.
Timu ya Ufaransa pia imekuwa ikiandamwa na virusi ambavyo vimewaathiri baadhi ya wachezaji wake lakini kocha Deschamp anaonekana kutolipa nafasi tatizo hilo licha ya kwamba baadhi ya wachezaji wake wamefungiwa vyumbani na wengine kufanya mazoezi peke yao.
“Tunajaribu kuendana na hali hiyo bila ya kulifanya lionekane jambo kubwa au kuangukia katika tukio hilo badala yake tunafanya kile kilicho na ulazima,” alisema.
Deschamps ambaye ndiye aliyekuwa nahodha wa timu ya Ufaransa iliyobeba taji la dunia mwaka 1998 na ndiye kocha aliyeipa timu hiyo taji la dunia mwaka 2018, aliulizwa kuhusu majeruhi katika kikosi chake, uwapo wa virusi na hamasa iliyotawala watu wengi ya kutamani Messi abebe taji na kumfanya yeye awe kama aliyeachwa peke yake.
“Kuna wakati naiona hali hiyo, lakini niko sawa kwa kuwa peke yangu, hilo wala halinisumbui, sina hofu yoyote wala wasiwasi wa mechi, unapojiandaa kwa mechi kama hii unatakiwa kuwa makini na kusimamia unachoamini, ingawa ni kweli kwamba kwenye mechi ya fainali hasa ya Kombe la Dunia kunakuwa na mengi ndani yake,” alisema.
“Ukweli ni kwamba lengo letu ni kuondoka na taji, najua Argentina na watu wengi duniani kote na pengine hata Ufaransa wanatumaini Lionel Messi atashinda taji la dunia lakini tunakwenda kufanya kila liwezekanalo kutimiza malengo yetu,” alisema.
Kimataifa Deschamps: Ya Messi hayanisumbui
Deschamps: Ya Messi hayanisumbui
Read also