Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ametoa angalizo kabla ya mechi yao na Simba akiwataka ka wachezaji wake kuwa makini zaidi kwenye mchezo huo kwani ndio ulioshikilia ubingwa wao msimu huu.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu NBC kwa sasa wapo kwenye maandalizi ya mchezo huo maarufu Dar Derby au Kariakoo Derby unaosubiriwa kwa hamu utakaopigwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam Jumapili hii.
Yanga itakuwa wageni wa Simba ingawa rekodi zinaonesha kuwa katika siku za karibuni imekuwa ikipata matokeo mazuri mbele ya Simba ambayo nayo kwa sasa imeimarika kwa kiasi kikubwa.
Katika kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo, Nabi amefuta mapumziko na sasa wapo kambini kuendelea na mazoezi kujiandaa na mchezo huo ambao umeshikilia hatima ya ubingwa wao kwa msimu huu.
“Ni mchezo mgumu wenye hadhi ya fainali sababu tukishinda tutakuwa na asilimia 85 ya kuwa mabingwa, nimewaeleza wachezaji wangu umuhimu wa ushindi na kuwataka kuzingatia kila tunachofanya mazoezini sababu hii ni mechi ya ubingwa,” alisema Nabi.
Kocha huyo ambaye amekipeleka kikosi cha Yanga hatua ya robo fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika ameeleza kuwa anajua mchezo huo utakuwa mgumu na wenye ushindani mkali kutokana na ubora wa kikosi cha Simba lakini ni lazima wapambane kuthibitisha kuwa wao ni bora.
Alisema anajua Simba wataingia kwa lengo la kutafuta ushindi ili kupunguza pengo la pointi nane lililopo kwa sasa lakini zipo mbinu mbadala ambazo amewapa wachezaji wake kwa ajili ya kuzifanyia kazi na kumpa pointi zote tatu kwenye mchezo huo.
Timu hizo zitaingia dimbani, Yanga ikiwa kileleni kwa pointi 68 dhidi ya Simba wanaoshika nafasi ya pili kwa pointi 60 huku zikiwa zimesalia mechi tano kabla ya kufungwa rasmi kwa pazia la ligi msimu huu.