Na mwandishi wetu
Mchanganyiko wa usajili wa wachezaji wa kigeni na wa ndani uliofanywa na timu ya Ihefu umeipa jeuri timu hiyo kiasi cha kujinasibu kuwa wachezaji hao watawabeba mno msimu ujao wa 2022/23 na kuonesha umahiri wao dhidi ya timu za Ligi Kuu ya NBC Bara.
Ihefu imepanda daraja kushiriki ligi hiyo baada ya kufanya hivyo pia msimu wa 2020/21 lakini ilishuka mwisho wa msimu huo baada ya kufanya vibaya na sasa imerejea upya.
Kocha Mkuu wa Ihefu, Zuberi Katwila amesema wanaamini usajili huo utawasaidia kwa kuwa ni wachezaji wenye viwango vizuri na uzoefu mkubwa katika ligi kutokana na ushindani waliounyesha huko walikopita.
Mpaka sasa timu hiyo ambao ni mabingwa wa Championship wamewasajili wachezaji Obrey Chirwa aliyekuwa Namungo, Nicolas Wadada na Never Tigere waliokuwa Azam, Said Makapu (Polisi Tanzania), Peter Mwalyanzi (Kagera Sugar), Juma Nyosso (Geita Gold) na wengine.
“Usajili huu si tu kwamba ni mkubwa ila ni wa wachezaji ambao wanafahamika na utatusaidia kutokana na uzoefu walionao na pia viwango walivyonavyo kuelekea kwenye ushindani mkali wa msimu ujao wa ligi maana kila timu imesajili vizuri.
“Na imefanyika hivyo baada ya tathmini yenye lengo la kutaka kufanya vizuri zaidi msimu ujao tofauti na wakati ule tulipopanda tukashuka, tunahitaji kusalia mwisho wa msimu na kama kutakuwa na mengine hiyo ni faida ya ziada kwetu,” alisema Katwila.
Soka Usajili waipa jeuri Ihefu
Usajili waipa jeuri Ihefu
Read also