Na mwandishi wetu
Timu ya Azam imeibuka na kuomba radhi kwa kipigo cha bao 1-0 walichopokea jana Jumatatu dhidi ya Ihefu katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Highland Estates, Mbeya.
Kocha Msaidizi wa Azam, Kali Ongalla alisema hajaridhishwa na kiwango kilichooneshwa na wachezaji wake na kuwataka kujirekebisha ili walichokionesha katika mechi hiyo kisijirudie katika mchezo ujao.
Alisema, licha ya matokeo hayo kumuumiza na kumpa majonzi lakini hawana budi kurudi na kujipanga kwa michezo inayokuja ili kufanya vizuri zaidi.
“Wachezaji wangu wamecheza kiwango kibaya sana, yaani hiki tulichokionesha naomba kisijirudie tena, tunahitaji kujirekebisha makosa yasijirudie kiasi hiki, hatukuwa vizuri uwanjani, tylijaribu kufanya mengi ya kimbinu lakini ilishindikana.
“Kiujumla nadhani tulishindwa kufuata mpango wetu mkakati, mwisho wa siku imetuangusha sana, hatukuwa kazini kama ilivyotarajiwa, kwenye kutengeneza nafasi hatukuwa vizuri pia, tunaomba msamaha, mashabiki wetu wanastahili kitu kizuri zaidi,” alisema Ongala.
Naye Kocha wa Ihefu, Zuberi Katwila alisema nidhamu ya wachezaji wake imesaidia wao kupata ushindi ikiwemo kujitahidi kutofanya makosa na mwisho Azam iliingia kwenye mfumo wao ndio maana walifanikiwa.
“Niwapongeze wachezaji kwa kufanya vizuri na kutuwezesha kupata ushindi, makosa hayakuwa mengi, muda wote tulikuwa makini kwa ajili ya kuhakikisha tunapata matokeo na mwisho nidhamu imesaidia kushinda,” alisema.
Ihefu imefanikiwa kuzifunga baadhi ya timu kubwa kama Yanga kwenye uwanja wake wa Highland Estate na sasa imeichapa Azam huku mechi ijayo ikitarajiwa kuumana na Simba.
Timu hiyo ambayo sasa inashika nafasi ya sita kwa pointi 33, pointi moja nyuma ya Geita Gold inayoshika nafasi ya tano, imekuwa ikionesha kiwango bora kwa siku za karibuni ikionekana ni ubora wa kikosi walichoboresha katika dirisha dogo la usajili wa Januari, mwaka huu.
Azam inashikilia nafasi ya nne kwa pointi 47 baada ya mechi 25, ikipambana kumaliza nafasi ya tatu dhidi ya Singida Big Stars wanaoshikilia nafasi hiyo wakiwa na pointi 48.