Na mwandishi wetu
Yanga, kesho Jumapili itakuwa na kibarua kigumu dhidi ya TP Mazembe katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika ikiwa imepania kupata ushindi wa pili mfululizo.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu NBC wataikabili Mazembe kwenye Uwanja wa TP Mazembe, Lubumbashi wakiwa tayari wameshafuzu hatua ya robo fainali hivyo hawana cha kupoteza zaidi ya kutaka ushindi ili wamalize wakiwa vinara katika kundi lao.
Yanga inaongoza Kundi D kwa pointi 10 sawa na US Monastir ya Tunisia huku Real Bamako ya Mali na Mazembe zikiwa zimeshaaga michuano hiyo kutokana na uchache wa pointi walizonazo.
Pamoja na TP Mazembe kutokuwa na nafasi ya kusonga mbele lakini watahitaji kushinda ili kuweka heshima na rekodi nzuri mbele ya Yanga hasa ukizingatia katika mchezo wa mzunguko wa kwanza Mazembe walifungwa mabao 3-1.
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi ameeleza kuwa jeshi lake lipo kamili kuikabili Mazembe kutokana na maandalizi waliyofanya kwa wiki mbili baada ya mchezo wao wa mwisho na Monastir.
“Tupo hapa kwa ajili ya kukamilisha mechi za makundi lakini lengo likiwa ni kupata ushindi dhidi ya TP Mazembe, ni mchezo mgumu hilo halina ubishi lakini tunataka kumaliza kwa kuweka rekodi ya kuifunga Mazembe mechi zote mbili,” alisema Nabi.
“Kama wachezaji wangu watacheza kwa kujituma na kufuata maelekezo tuliyopeana mazoezini ninaamini uwezo wa kupata pointi tatu upo tena mkubwa lakini tutacheza kwa nidhamu kubwa sababu Mazembe si timu dhaifu kama watu wanavyowachukulia,” alisema Nabi.
Baada ya kuvuka hatua ya makundi malengo ya Yanga ni kufika nusu fainali na ikiwezekana kutwaa ubingwa wa Afrika na hiyo ni kutokana na ubora wa kikosi chao na mbinu bora kutoka benchi lao la ufundi linaloongozwa na Nabi.