Na mwandishi wetu
Mshambuliaji kinara wa Simba Queens, Jentrix Shikangwa (pichani) ametajwa kuwa mchezaji bora wa mwezi Machi huku mchezaji mkongwe wa JKT Queens, Stumai Abdallah akiibuka mchezaji bora wa mwezi Aprili kwenye Ligi Kuu ya Wanawake msimu huu.
Wawili hao wametajwa leo Jumanne kuibuka vinara wa tuzo hizo kutokana na viwango walivyoonesha katika mechi walizocheza kwenye timu zao katika miezi hiyo.
Shikangwa raia wa Kenya anayeongoza kwa kufunga mabao 14 mpaka sasa, katika mwezi huo alifunga mabao matatu katika mechi tatu alizocheza.
JKT inayoongoza ligi kwa pointi 37 ikionesha kiwango kikubwa msimu huu mpaka sasa, Stumai anakuwa mchezaji wao wa pili kuchukua tuzo hiyo ikiwa tayari zimeshatolewa tano mpaka sasa.
Mchezaji mwingine wa JKT, Donisia Minja anayeshikilia nafasi ya pili kwa mabao 12 aliiweka kibindoni tuzo ya mchezaji bora mwezi Februari.
Upande wa Simba inayoshikilia nafasi ya pili kwa pointi 36, hii ni tuzo yao ya tatu baada ya awali mwezi Desemba na Januari kuchukuliwa na Opa Clement aliyetimkia klabu ya Besiktas ya Uturuki hivi karibuni.
Soka Jentrix, Stumai watwaa tuzo
Jentrix, Stumai watwaa tuzo
Read also
