Na mwandishi wetu
Bondia wa ngumi za kulipwa nchini, Hassan Mwakinyo ameeleza kutoridhishwa kupanda ulingoni kesho Ijumaa kuzichapa na Julius Indongo wa Namibia badala ya Mkenya, Rayton Okwiri.
Awali, pambano hilo la kuwania mkanda wa IBA Intercontinental lilitangazwa kuwa Mwakinyo atazichapa na Okwiri kabla ya jana kuelezwa kuwa Okwiri ameumia akiwa kwenye maandalizi na nafasi yake kuchukuliwa na Indongo.
Pamoja na kutoridhishwa huko, Mwakinyo amesema hatoacha kupanda ulingoni ingawa hakikuwa kitu kinachotarajiwa na mashabiki wake kuelekea pambano hilo litakalopigwa kwenye Ukumbi wa Ubungo Plaza, Dar es Salaam.
“Binafsi sijaridhishwa na mabadilko haya lakini ni bora kugawa chakula kilichokwishaandaliwa kuliko kukitupa, natumai washabiki zangu ni waungwana na kwa pamoja mtaelewa mabadiliko haya,” alisema Mwakinyo au Champez.
Wawili hao watapambana katika pambano hilo litakalokuwa na raundi 10 huku yakitarajiwa kupigwa mapambano mengine saba ya utangulizi.
Indongo ambaye ni bingwa wa zamani wa mikanda ya WBA, IBF na IBO amewahi kupigana na Mwakinyo Septemba 3, mwaka juzi na Mwakinyo kushinda kwa TKO raundi ya nne.