Na mwandishi wetu
Kocha mpya wa Tanzania Prisons, Mohamed Abdallah Bares ameahidi kuinusuru timu hiyo na janga la kushuka daraja kwa kushinda mechi zao tisa zilizobaki kwenye Ligi Kuu NBC.
Kocha huyo mshindi wa Kombe la Mapinduzi 2023 akiwa na timu ya Mlandege, amejiunga na Maafande hao akichukua mikoba ya Patrick Odhiambo raia wa Kenya aliyefutwa kazi hivi karibuni kutokana na mwenendo mbaya wa timu hiyo.
Bares ameeleza kufahamu ugumu wa jukumu alilojivika lakini atapambana kwa kushirikiana na uongozi ili kuhakikisha timu hiyo inapata matokeo mazuri katika mechi zilizosalia kabla msimu kumalizika.
“Nafurahi kurudi tena Prisons, hii inaonesha namna gani viongozi wana imani na mimi ingawa hakuna ubishi kwamba kazi hii ni ngumu kutokana na nafasi ambayo timu ipo lakini nitajitahidi kupambana kwa kushirikiana na wenzangu kuhakikisha tunabaki ligi kuu,” alisema Bares.
Kocha huyo ameeleza kuwa matatizo la timu hiyo ni madogo sana ikiwemo kupata matokeo, atajitahidi kuhakikisha hilo linawezekana sababu ameshuhudia baadhi ya mechi za timu hiyo inacheza vizuri na wana wachezaji wapambanaji wa kutosha.
Alisema kitu cha msingi anahitaji kuwepo kwa umoja ndani ya timu pamoja na sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wao anaamini hakuna kitakachoshindikana katika mechi zilizobaki.
Tanzania Prisons inashika nafasi ya 12 kwenye msimamo wa ligi wakikusanya pointi 21 katika idadi kama hiyo ya mechi walizocheza mpaka sasa.