Na mwandishi wetu
Azam FC imeianza Ligi Kuu NBC vizuri kwenye uwanja wake wa nyumbani wa Azam Complex kwa kuichapa Mbeya City mabao 2-0 wakati Yanga nayo ikianza kwa kuinyuka Pamba Jiji mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Mechi hizo za mwanzo za ligi hiyo zimechezwa Jumatano hii Septemba 24, 2025 ambapo Azam chini ya kocha wao mpya, Florent Ibenge walianza kuziona nyavu za Mbeya City kwa bao la dakika ya 32 lililofungwa na Nassor Saadun.
Bao hilo lilitokana na shambulizi lililotokana na mpira wa kona lililoanzishwa na Feisal Salum au Fei Toto na mpira kumfikia Abdul Sopu aliyetoa pasi iliyozaa bao hilo lililodumu hadi mapumziko.
Kipindi cha pili Azam walikianza kwa kasi na kuandika bao la pili katika muda usiozidi dakika moja baada ya kuanza kipindi hicho mfungaji akiwa Fei Toto aliyeitumia pasi ya mchezaji bora wa mechi hiyo, Baraket lhmidi.
Kwa upande wa Yanga wao walianza kuzichana nyavu za Pamba dakika ya 45 kwa bao la nyota wao mpya, Lassine Kouma aliyefunga kwa kichwa baada ya kuruka juu na kuuwahi mpira wa kona iliyochongwa na Edmund John.
Kipindi cha pili kocha wa Yanga, Romain Folz alifanya mabadiliko kadhaa yaliyoonekana kuipa uhai timu hiyo na kufanikiwa kupata bao la pili lililofungwa na mchezaji bora wa mechi hiyo, Maxi Nzengeli dakika ya 61 akiitumia pasi ya aliyekuwa beki wa Simba, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Junior’.
Kasi ya Yanga iliendelea ambapo wapinzani wao Pamba Jiji wakajikuta wakiwa na kazi ngumu ya kujihami na hata walipojaribu kufanya mashambulizi hayakuweza kuleta athari zozote kwenye lango la Yanga.
Ikiwa imebakia dakika moja mpira kumalizika, Yanga waliandika bao la tatu lililofungwa na Mudathir Yahya ambaye aliitumia krosi iliyochongwa na Pacome Zouzoua.
Kimataifa Azam, Yanga mwanzo mzuri
Azam, Yanga mwanzo mzuri
Read also
