Manchester, England
Kocha wa Man City, Pep Guardiola amemshauri mshambuliaji wake tishio Erling Haaland kuweka fikra zake katika kupumzika na kurahisisha mambo zaidi kuliko kufikiria kufunga magoli.
Man City leo Jumanne itaingia dimbani kuendelea na mbio za kulitetea taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya itakapokuwa mgeni wa FC Copenhagen katika mechi ya kwanza ya hatua ya 16 bora.
Haaland ndio kwanza amerejea baada ya kuwa majeruhi kwa takriban miezi miwili na Pep anadhani mchezaji huyo amekuwa na uchu wa kuendelea kuzifumania nyavu kwa mara nyingine.
Tayari mshambuliaji huyo ameshaonesha makali yake katika mechi ya Ligi Kuu England (EPL) dhidi ya Everton na matarajio ya kuendelea kutamba ni makubwa kwake na kwa mashabiki wa timu hiyo.
“Ana mtazamo wa kuzifumania nyavu lakini tusisahau kwamba alikuwa nje kwa miezi miwili, kurudi kwenye ubora wake si jambo rahisi, ni mpambanaji mkubwa anayetaka kufunga magoli, ni sawa hilo tunalifahamu lakini atulie,” alisema Pep.
“Kama hatutafunga leo au hatofunga katika dakika 10 ni sawa, katika harakati hizo atakuwa mwenye kujaribu kwa sababu timu wakati wote huwa inashinda inapokabiliana na mwenendo mbaya,” alisema Pep.
Pep alisema kwamba anajua anaonekana kama analalamika kuhusu mchezaji huyo lakini hilo ni jambo lililo wazi, hasa unapojiuliza idadi ya mechi alizocheza na mabao aliyofunga, ukimuangalia huoni tatizo.
“Kwangu mimi kama hatofunga kesho (leo Jumanne) au siku inayofuata au hata wiki ijayo kwangu si jambo kubwa,” alisema Pep.
Haaland alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu uliopita akiwa na mabao 12 wakati Man City ilipobeba taji hilo kwa mara ya kwanza na ndiye aliyekuwa kinara wa mabao katika EPL msimu uliopita.
Mechi za Ligi ya Mabingwa Leo Jumanne
FC Copenhagen v Man City
RB Leipzig v Real Madrid
Mechi za Ligi ya Mabingwa Ulaya kesho Jumatano
Lazio v Bayern Munich
PSG v Real Sociedad