Na mwandishi wetu
Beki na nahodha wa Simba, Mohamed Hussein ‘Zimbwe Jr’ hatimaye ametangaza kuachana na timu hiyo aliyoitumikia kwa takriban miaka 11 huku akihusishwa na mipango ya kuhamia Yanga.
Hatua ya Zimbwe kuachana na Simba imekuja baada ya kuwapo habari katika siku za karibuni kuwa amemaliza mkataba na uongozi Simba haukuwa na nia ya kumpa mkataba mpya.
Hadithi ya beki huyo mahiri wa kushoto ambaye pia anaichezea timu ya taifa ya Tanzania, kuachana na Simba ilianzia kwenye mitandao ya kijamii na kuibua mijadala miongoni mwa mashabiki.
Baada ya hapo kukawa na habari ya mchezaji huyo kuondoa utambulisho wa klabu ya Simba katika akaunti zake za mitandao ya kijamii jambo lililotoa ishara kwamba kilichosemwa kuhusu mchezaji huyo kina dalili zote za ukweli.
Habari kubwa ya karibuni ni ile ya mchezaji huyo kuaga akiushukuru uongozi, benchi la ufundi, wafanyakazi wa klabu na mashabiki kwa kumuunga mkono kipindi chote alichokuwa na timu hiyo.
Na ingawa bado taarifa za kuondoka kwa beki huyo hazijawa rasmi lakini habari kubwa kwa sasa ni kuhusu timu anayojiunga nayo baada ya Simba huku mahasimu wao, Yanga wakipewa nafasi kubwa kumsajili beki huyo.
Zimbwe amecheza Simba kwa mafanikio akihusika kikamilifu kuipa mataji ya ndani na kushiriki kikamilifu kwenye michuano ya klabu Afrika tangu ajiunge na timu hiyo mwaka 2014 akitokea Kagera Sugar.
Kwa kipindi chote cha miaka 11 aliyoichezea Simba, Zimbwe ambaye pia alifahamika kwa jina la Tshabalala, amekuwa mchezaji mwenye uhakika wa namba kikosi cha kwanza.
Soka Zimbwe Jr aaga Simba
Zimbwe Jr aaga Simba
Read also
