Na mwandishi wetu
Kocha mkuu wa Yanga, Miguel Gamondi amesema kwamba wanafahamu ugumu ulio mbele yao katika mechi dhidi ya Mamemelodi Sundowns lakini watatafuta matokeo ugenini.
Kauli ya Gamondi imekuja wakati Yanga ikiwa imetua salama jijini Johannesburg, Afrika Kusini kwa mchezo huo ambao ni wa marudiano wa robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Yanga itakipiga na Mamelodi Aprili 5, mwaka huu kwenye Uwanja wa Loftus Versfeld, Pretoria ikitafuta sare ya mabao au ushindi wa aina yoyote ili kufuzu hatua ya nusu fainali kwa mara ya kwanza baada ya matokeo ya 0-0 kwenye mchezo wa awali uliopigwa Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam.
“Mchezo ni mgumu, nafikiri mchezo utakuwa na presha inayofanana maana Sundowns wana presha ya kutaka kuingia nusu fainali sababu ni miongoni mwa wanaopewa nafasi ya kutwaa ubingwa.
“Na wao pia wanataka kushinda, washiriki kwenye michuano ya Klabu Bingwa Dunia lakini nategemea utakuwa mchezo wa mbinu na tutapambana kupata bao ugenini sababu kama nafasi tunatengeneza, tunachohitaji kuendelea kushikamana, nikiwaamini vijana wangu, natumai tutaingia nusu,” alisema Gamondi.
Kocha huyo raia wa Argentina pia alizungumzia uwezekano wa mabadiliko ya kikosi katika mchezo huo kutokana na maendeleo mazuri waliyonayo majeruhi wake.
Wachezaji majeruhi wa Yanga ni Pacome Zouzoua, Kouassi Yao na Khalid Aucho ambao wote walikosekana katika mchezo wa kwanza kutokana na kuwa na majeraha mbalimbali.