Na Jonathan Haule
Una mpenzi na una matarajio makubwa kwake, ghafla anakukataa, unafikiria kujiua, kwa nini? Unajua Kanye West rapa maarufu na tajiri amewahi kukataliwa? Unajua Ben Affleck, staa wa filamu na tajiri amewahi kukataliwa? Vipi wewe huna chochote unataka kujiua kisa mpenzi amekukataa…
Matukio ya watu kujiua kwa sababu ya kukataliwa na wapenzi wao yamekuwa yakisikika mara kwa mara, na hapa ndipo baadhi yetu tunapoanza kujiuliza, kulikoni mtu anafikia hatua ya kutaka kujia kwa sababu tu amekataliwa, lakini nini suluhisho la tatizo hili?
Wataalam wengi wa saikolojia wanasema kwamba mtu anapofikia uamuzi wa kutaka kujiua maana yake ni kwamba amekosa suluhisho jingine na kuona kitu pekee anachoweza kufanya ni kujiua, kwa maana nyingine mtu huyu amekosa msaada, amekosa mtu wa kumsaidia kufikiria tofauti.
Kwa hiyo jamii ina kazi ndogo ya kuwafikirisha tofauti wale wenye mawazo au wenye kuamini kwamba kujiua ndilo suluhisho pekee la matatizo ya mahusiano yanayowakabili, kuwafanya waamini kwamba wao si wa kwanza kukataliwa, wapo watu wengi maarufu na matajiri na masikini waliokataliwa na hapana shaka wanaendelea kukataliwa.
Nimeanza kwa kumtaja Ben Affleck, staa wa filamu ambaye alikuwa katika mapenzi moto moto na mwanamuziki na staa mwenzake wa filamu, Jennifer Lopez au J.Lo, kutokana na umaarufu wa wapenzi hawa, vyombo vya habari viliwabatiza jina la ‘Super Couple’ lakini wakati umma ukijadili siku ya ndoa ya ‘Ma-Super Couple; hawa ghafla J.Lo akafuta uchumba na mipango ya ndoa, akamuacha Ben Affleck.
Nini kilitokea? Ben Affleck akakubali matokeo na haikuchukua muda akampata mpenzi mwingine Jennifer Garner, wakafunga ndoa, wakapata watoto na kuendelea na maisha yake mapya. J.Lo naye baadaye akapata mume wakafunga ndoa na kupata watoto wawili mapacha.
Mtu mwingine aliyekutana na janga la kuachwa ni Kanye West, rapa tajiri ambaye ndoa na mapenzi moto moto kati yake na mwanamitindo na staa wa vipindi vya televisheni Kim Kardashian imevunjika licha ya umaarufu waliokuwa nao na kuwa kwenye vyombo vya habari kila wakati.
Kanye amekubali matokeo ya kuachwa na anaendelea na maisha yake kama kawaida kama ambavyo Kim naye anaendelea na staili yake ya maisha kama kawaida. Vipi wewe unawaza kujiua kisa mwanamke au mwanaume amekukataa!
Miaka ya 2000 mwanzoni mwanasoka maarufu duniani, Ronaldo de Lima (si Cristiano Ronaldo) alikataliwa na mrembo mmoja wa Ufaransa wakati akijiandaa kukamilisha masuala ya uchumba, mrembo huyo alifuta mipango hiyo dakika za mwisho wakati dunia yote ya soka ilishaaminishwa kwamba mpenzi wa Ronaldo anaishi Ufaransa. Nini alikifanya Ronaldo, alikubali matokeo na kuendelea na mapambano yake kwenye soka.
Unapoachwa usijenge zile fikra kwamba Jennifer au Joyce ndio kila kitu au hakuna kama Jennifer au Joyce, hapana, hayo ni maneno tu ya kuridhishana kwenye mapenzi lakini hayana uhalisia wowote. Usimsikie mtu anamwambia mpenzi wake, ‘wewe ndio moyo wangu, bila wewe sipumui au kwa msisitizo anaweza kumwambia; “You are my everything (wewe ni kila kitu kwangu),’ haya ni maneno tu, ni porojo za kunogesha mapenzi, ni kudanganyana kunakohalalishwa na wapendanao pale mapenzi yanapokolea lakini kimsingi hakuna mtu aliyebeba moyo wa mwingine.
Kina Joyce, Jennifer na wengineo wako wengi, anapokukataa mmoja jua wapo wengine wengi, wapenzi wetu hawa ni kama samaki baharini, unapomkosa mmoja, angalia namna ya kuvua mwingine, huna sababu ya kufikiria kujiua kama ambavyo Ben Affleck aliachwa na Jennifer akampata Jennifer mpya, na kwako inawezekana kumpata Jennifer, Joyce, John au Jonathan mwingine. Achana na wazo la kujiua.
Nimetoa mfano wa matajiri walioachwa lakini wakakubali ili kudhihirisha kwamba suala la kuachwa si lazima lihusishe uwezo wa mtu kifedha, tajiri naye anaweza kuachwa, hivyo hata wewe masikini unapoachwa kubali matokeo, tajiri anayeachwa huenda anaumia kuliko wewe masikini kwa sababu anateswa na hali ya kutoamini kwamba nguvu ya pesa zake si lolote kwenye mapenzi.
Niliwahi kumtolea mtu mmoja mfano wa Ronaldo alivyokubali kuachwa na kuendelea na maisha yake ya soka, mtu huyu ndiye aliyenifungua kuhusu umuhimu wa kukubali matokeo na kuangalia mengi mengine, lakini akasema kwamba watu wa mpira wana faida moja katika jambo hili, wamekua katika somo la kukubali matokeo.
Akasema Ronaldo na wenzake wa timu ya Brazil walilikosa Kombe la Dunia mwaka 1998 nchini Ufaransa licha ya dunia ya soka kuamini kwamba wanalibeba taji hilo na hivyo mshtuko wa kulikosa ulikuwa mkubwa mno lakini yeye na wenzake walikubali matokeo, wakajiandaa na mwaka 2002 wakalipata taji hilo hilo walilolikosa Ufaransa.
Kwa hiyo na wewe mwenzangu unapoachwa hata kama umewekeza kwa kiasi gani kwa mpenzi wako, kwanza kubali matokeo, uwekezaji wako uliofanya haufikii hata robo ya uwekezaji wa Kanye West kwa Kim, uwekezaji wako wa kumlipia mrembo ada au kumnunulia kigari haufikii hata kidogo uwekezaji wa Ben Affleck kwa J.Lo, sasa kwa nini kuachwa kwako liwe jambo kubwa na la kukufanya uone hakuna zaidi ya kujiua.
Unachoweza kufanya baada ya kuachwa ni kupambana na mambo yako kwa bidii zaidi, kuangalia mbele na kuanza taratibu kumfikiria mpenzi mwingine ambaye bila shaka utampata na huenda ukamfurahia kuliko yule aliyekuacha au hata huyo huyo aliyekuacha anaweza kubadili mawazo mkarudiana kama ambavyo imetokea kwa Ben Affleck na J.Lo.
Ben Affleck na J.Lo waliachana miaka 17 iliyopita lakini hivi karibuni wamerudiana na kwa sasa wanajirusha na kula maraha hakuna mfano, leo hii wakiwa wawili Ben Affleck anaonekana mkononi akiwa na saa ile ile ya thamani aliyopewa zawadi na J.Lo mwaka 2002. Inawezekana hata kwako, achana na fikra za kujiua.
Tukutane juma lijalo ambapo tutajadili namna kuachwa kunavyowafanya watu kuchukua maamuzi mengine mabaya mbali na yale ya kutaka kujiua.
green.sports82@gmail.com
Mahusiano Kwanini utake kujiua mpenzi anapokukataa?
Kwanini utake kujiua mpenzi anapokukataa?
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
