Na mwandishi wetu
Klabu ya Yanga imeeleza iko mbioni kufunga usajili wake wa dirisha dogo kwa kushusha wachezaji wawili wa kimataifa watakaokuwa na tija kwa timu hiyo kuelekea mwisho wa msimu huu.
Mpaka sasa Yanga imesajili mchezaji mmoja, kiungo wa kati Mudathir Yahya kwenye dirisha hili linalotarajia kufungwa Januari 15, mwaka huu.
Ofisa Habari wa Yanga, Ali Kamwe alisema jana kuwa kwa siku chache zilizobakia kabla ya kufungwa kwa dirisha hilo watakuwa wamekamilisha sajili hizo kwani mazungumzo na walipofikia ni zaidi ya asilimia 90 na imebaki sehemu ndogo kukamilisha mpango huo.
“Usajili wa Mudathir kila mmoja ameuona, ni usajili wenye manufaa kwetu tangu awali benchi ililiona hilo na niwaambie tu mashabiki na wapenzi wa Yanga kuwa bado hatujamaliza kufanya usajili.” Kamwe.
“Ndani ya siku hizi chache zilizobaki, tunamalizana na wachezaji wawili wa kimataifa na tutawatangaza muda si mrefu maana tupo kwenye mazungumzo na timu zao na mazungumzo na wachezaji binafsi ambayo tumefikia zaidi ya asilimia 90 kukamilisha dili hizo,” alisema Kamwe.
Licha ya Kamwe kutotaja majina ya wachezaji wanaowawania lakini duru mbalimbali zinaeleza kuwa miongoni mwa wachezaji hao wanaomalizana na Yanga ni Kennedy Musonda wa Power Dynamos ya Zambia.
Yanga inamuhitaji mchezaji huyo baada ya kuelezwa kuachana na Herritier Makambo huku Lazarous Kambole akionekana ameonesha kiwango cha kawaida kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi, Zanzibar na hivyo kulishawishi benchi kutafuta wa kusaidiana na Fiston Mayele.
