Na mwandishi wetu
Mudathir Yahya leo Jumatano ameiokoa Yanga kugawana pointi na Namungo baada ya kufunga bao pekee la ushindi katika mechi ya Ligi Kuu NBC iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Mudathir aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Clement Mzize alifunga bao hilo katika dakika ya 88 akimalizia pasi ya Aziz Ki ambaye aliunganishiwa mpira na Kouassi Yao kutoka upande wa kulia wa Yanga.
Bao hilo lilikuja baada ya Namungo kuonesha uhai kwa muda mrefu wa mchezo kwa kujihami vizuri, kuitibulia Yanga na wakati mwingine kufanya mashambulizi yaliyoibua hofu langoni mwa wapinzani wao.
Kipindi chote cha kwanza, Namungo inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, Cedric Kaze ilicheza vizuri, haikuonekana kuwa dhaifu mbele ya Yanga ambayo imetoka kushindi mabao matano kila mechi katika mechi zake mbili zilizopita za ligi hiyo.
Namungo wakati mwingine ilionekana kuwa tishio kwenye lango la Yanga kiasi cha kutoa dalili za kumaliza mchezo kwa sare au hata kuibuka na ushindi ambao ungekuwa wa kwanza dhidi ya Yanga tangu timu hiyo ipande daraja na kushiriki ligi kuu.
Dakika za 78 na 79 Namungo walifanya mashambulizi mawili ambayo yaliwaweka katika hali ya hofu mashabiki wa Yanga ambao baadhi yao walianza kupoteza matumaini ya kutoka na ushindi katika mechi hiyo.
Katika shambulizi la kwanza, winga wa zamani wa Simba, Shiza Kichuya akiwa upande wa kushoto karibu na lango la Yanga aliunasa mpira na kupiga shuti dhaifu ambalo ilikuwa kama kumpasia kipa Diarra aliyeutuliza mpira kwenye himaya yake kiurahisi.
Baada ya shambulizi hilo Namungo walirudi tena langoni mwa Yanga ambapo Buswita akiwa katika nafasi nzuri aliunasa mpira na kupiga shuti kubwa ambalo halikuwa na madhara yoyote langoni mwa Yanga.
Yanga nao walifanya mashambulizi kadhaa ikiwamo lile la dakika ya 56 baada ya Pacome Zouazoua kuinasa pasi ya Aziz Ki na kumchungulia kipa wa Namungo, Deo Munishi Dida lakini shuti la Zouazoua lilitua mikononi mwa Dida.
Dakika ya 68 kwa mara nyingine Yanga walifanya shambulizi baada ya Aziz Ki kuambaa na mpira na kuwazidi ujanja mabeki wa Namungo kabla ya kufumua shuti la chinichini lakini kwa mara nyingine Dida alionesha umahiri wake kwa kuinyima Yanga bao.
Kwa ushindi huo Yanga imeendelea kujiimarisha kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo ikiwa imefikisha pointi tisa na mabao 11 katika mechi tatu. Ligi hiyo itaendelea kesho Alhamisi kwa mechi kati ya Simba na Coastal Union na Azam FC dhidi ya Singida Fountain Gate au Singida Big Stars.
Soka Mudathir aokoa jahazi Yanga
Mudathir aokoa jahazi Yanga
Read also