London, England
Klabu ya Manchester City inatarajia kukumbana na rungu la FA kwa kitendo cha mashabiki wake kuvamia uwanja siku ambayo timu hiyo iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Aston Villa katika mechi iliyoihakikishia timu hiyo taji la Ligi Kuu England msimu wa 2021/22.
Maelfu ya mashabiki wa City walivamia katikati ya Uwanja wa Etihad kufurahia taji lao la nne la Ligi Kuu England katika msimu wa tano na sasa mabosi wa klabu hiyo wamepewa na FA hadi Agosti 25 kujibu madai hayo.
Katika tukio hilo mashabiki wa Man City walizua tafrani kwa namna walivyokuwa wakishangilia taji hilo katikati ya uwanja huku kukiwa na habari kwamba kipa wa Villa, Robin Olsen alijikuta akivamiwa wakati mwamba wa goli moja ukivunjwa.
Taarifa ya FA ilieleza, “Inadaiwa kwamba mara baada ya filimbi ya kumaliza mchezo kupulizwa, Manchester City walishindwa kuhakikisha mashabiki wao na watu wengine wanaoaminika kuwa mashabiki wao au wafuasi wao hawafanyi yasiyo nje ya utaratibu na kujiepusha na tabia zisizofaa wakati wakiingia eneo la kati la uwanja.”
Mwezi Mei, kipindi ambacho mechi hiyo ilichezwa watu wawili walikamatwa wakihusishwa na matukio ya kuvamia uwanja wakati Polisi wa Manchester walisema mwezi uliopita kwamba bado wanachunguza matukio kadhaa ya kihalifu ikiwamo ya jinai na uharibifu.
Man City ilifunga mabao matatu katika dakika tano baada ya kuwa nyuma kwa mabao 2-0 zikiwa zimebaki dakika tano mpira kumalizika na hatimaye kuibuka na ushindi wa mabao 3-2 na kulitwaa taji hilo kwa kumzidi mshindani wake wa karibu, Liverpool kwa tofauti ya pointi moja.

Vita ya Man City na Liverpool katika kuliwania taji la Ligi Kuu England msimu wa 2021/22 ilikuwa kali na iliyojaa ushindani na kabla ya mechi ya mwisho kuchezwa mashabiki wa timu zote walikuwa na hali ya wasiwasi kuhusu matokeo ya mechi zao za mwisho.
Inaaminika mashabiki wa City walijawa na furaha si kwa sababu ya kulibeba taji hilo tu bali mazingira ya ushindani na namna walivyofanikiwa kulibeba taji ndiyo yaliyowafanya kujawa furaha isiyo kifani hadi kuvamia uwanja, kwanza ni namna walivyovuruga matumaini ya Liverpool kubeba taji hilo.
Namna ushindi wao ulivyopatikana katika dakika 15 za mwisho ulitosha kuwafanya wawe na furaha isiyo kifani, hasa ushindi wenyewe umepatikana wakiwa nyumbani Etihad hivyo hawakusita kuingia katikati ya uwanja kufurahia ubingwa kwa raha zao.
Kutokana na mazingira ya vurugu hizo uwezekano wa klabu ya Man City kulikwepa rungu la FA ni mdogo badala yake klabu hiyo itajikuta ikitozwa faini, uwanja kufungiwa kama hayo mawili yatashindikana basi itapewa japo onyo kali.
