New York, Marekani
Mshambuliaji wa zamani wa Man Utd, Wayne Rooney amejitosa katika sakata la usajili wa Cristiano Ronaldo akiitaka timu hiyo kuachana na mchezaji huyo kama inataka kujenga timu yenye mafanikio.
Ronaldo mwenye umri wa miaka 37 alisajiliwa Man Utd msimu uliopita akitokea Juventus lakini sasa anataka kuondoka kwa kinachodaiwa kuwa ni kukosa nafasi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya ingawa kocha mpya wa timu hiyo, Erik ten Hag bado anamtaka mchezaji huyo ambaye ana mwaka mmoja katika mkataba wake.
“Nafikiri United inatakiwa kumuacha Cristiano Ronaldo aondoke, si kwamba Ronaldo hawezi kucheza katika timu ya Ten Hag, hapana, anaweza kucheza kwenye timu yoyote,” alisema Rooney ambaye kwa sasa ni kocha wa timu ya DC United inayoshiriki Major League Soccer nchini Marekani.
“Ronny wakati wote anaweza kufunga magoli, lakini kwa mtazamo wangu ni kwamba United haiko tayari kwa changamoto ya kupigania taji kwa sasa, hivyo lengo ni lazima liwe kuijenga timu ya kupigania taji la ligi kwa miaka mitatu au minne ijayo na kwa jambo hilo ni lazima kuwe na mipango.”
Man Utd ilianza mtihani wake wa kwanza wa Ligi Kuu England msimu wa 2022/23 jana Jumapili kwa kuumana na Brighton, mechi ambayo Ronaldo alisugua benchi akiishuhudia timu hiyo ikilala kwa mabao 2-1 kwenye dimba la Old Trafford.
Rooney hata hivyo alisema kwamba ana matumaini, Ten Hag ataweza kutengeneza mfumo wa uchezaji ulio wazi katika timu hiyo, “Sijaweza kujua nini wanakifanya kuhusu mpango wao kiuchezaji au kuijua aina yao ya uchezaji ila nafikiri moja ya mambo makubwa mtayaona kutoka kwa Ten Hag, anajitahidi kuweka alama yake katika mfumo wa uchezaji.”
Kimataifa Muacheni Ronaldo aondoke- Rooney
Muacheni Ronaldo aondoke- Rooney
Read also
