Casablanca, Morocco
Kocha wa timu ya Taifa ya Morocco, Walid Regragui ametaja majina ya wachezaji 26 watakaoenda Qatar kwenye fainali za Kombe la Dunia ambapo amemjumuisha, Hakim Ziyech, winga anayehaha kupata namba katika kikosi cha Chelsea.
Ziyech kwa msimu huu amecheza mechi mbili tu na Chelsea lakini ni mmoja wa wachezaji tisa ambao wanaiwakilisha Morocco kwenye fainali za Kombe la Dunia kwa mara ya pili mfululizo baada ya kuwamo katika timu iliyoshiriki fainali hizo nchini Urusi mwaka 2018 na kutolewa katika hatua ya makundi.
Ziyech mbali na kuwa na wakati mgumu Chelsea lakini kwenye timu ya Morocco aliwahi kuwa chanzo cha mzozo kati ya shirikisho la soka la nchi hiyo na kocha wa zamani wa timu hiyo, Vahid Halilhodzic baada ya mchezaji huyo pamoja na beki wa Bayern Munich, Noussair Mazraoui kuachwa katika kikosi hicho kwa utovu wa nidhamu.
Halilhodzic licha ya kushinikizwa na shirikisho hilo kuwapa nafasi wachezaji hao katika kikosi chake lakini alishikilia msimamo wa kuwakataa na inaaminika hiyo ndiyo sababu mojawapo ya kocha huyo kutimuliwa na majukumu hayo kukabidhiwa, Regragui ambaye Mei mwaka huu alibeba taji la Ligi ya Mabingwa Afrika akiwa na timu ya Wydad Casablanca ya Morocco.
Wachezaji wengine waliopewa nafasi na Regragui ni beki wa West Ham, Nayef Aguerd ambaye pia amekuwa nje ya uwanja kwa takriban miezi mitatu akiuguza maumivu ya enka pamoja na mshambuliaji wa Sevilla, Youssef En-Nesyri ambaye naye mambo yake si mazuri ndani ya klabu hiyo msimu huu.
Kikosi kamili cha Morocco ambayo imepangwa Kundi F na timu za Ubelgiji, Canada na Croatia ni kama ifuatavyo…
Makipa Yassine Bounou (Sevilla), Munir El Kajoui (Al Wehda) na Ahmed Reda Tagnaouti wa Wydad Casablanca.
Mabeki Nayef Aguerd (West Ham United), Yahia Attiat Allah (Wydad Casablanca), Badr Benoun (Qatar SC), Achraf Dari (Stade Brest), Jawad El Yamiq (Real Valladolid), Achraf Hakimi (Paris St Germain), Noussair Mazraoui (Bayern Munich) na Romain Saiss wa Besiktas.
Viungo: Sofyan Amrabat (Fiorentina), Selim Amallah (Standard Liege), Bilal El Khannouss (Racing Genk), Yahya Jabrane (Wydad Casablanca), Azzedine Ounahi (Angers) na Abdelhamid Sabiri wa Sampdoria.
Washambuliaji: Zakaria Aboukhlal (Toulouse), Soufiane Boufal (Angers), Ilias Chair (Queens Park Rangers), Walid Cheddira (Bari), En-Nesyri (Sevilla), Abde Ezzalzouli (Osasuna), Abderrazak Hamdallah (Al Ittihad), Amine Harit (Olympique Marseille) na Ziyech wa Chelsea.
Kimataifa Ziyech wa Chelsea aitwa kikosini Morocco
Ziyech wa Chelsea aitwa kikosini Morocco
Green SportsAuthor / Greensports Media LTD
Greensports author
Read also
