Rio de Janeiro, Brazil
Mwanasoka gwiji wa zamani wa Brazil, Pele alipatwa na ugonjwa wa korona na mapigo ya moyo hayakuwa vizuri kabla ya kulazwa hospitali Jumanne iliyopita. Mtoto wake amethibitisha hilo.
Pele, mwenye umri wa miaka 82 sasa alipimwa na kukutwa na korona mwezi uliopita na alipewa tiba ya kupunguza maumivu na homa lakini korona ndio sababu kuu iliyomfanya apelekwe hospitali.
“Wiki kama tatu hivi zilizopita, alipatwa na korona, amepata chanjo ya kinga zote lakini kwa sababu ya tiba ya saratani amekutwa pia na matatizo kwenye mapafu na ndio maana alipelekwa hospitali, tatizo limekuwa kubwa kwa sababu ya umri wake pamoja na tiba anayofanyiwa ya saratani,” alisema Kely Nascimento wakati akizungumza na kituo kimoja cha televisheni.
Taarifa ya familia pia ilieleza kwamba Pele alipelekwa hospitali kwa sababu huko anapata uangalizi mzuri lakini hayuko ICU (chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu) “kwa kuwa ni mtu ambaye kiafya hajakaa sawa ni vizuri kwake kuwa hospitali, si haki kuanza kusema yuko katika hali mbaya. Kwa tiba anayopata si kwamba ana hali mbaya sana.”
“Hali si mbaya sana, mtuamini sisi kuliko mtu mwingine yeyote, hatutaki hali ifike huko kubaya, ni kweli kwamba kuna siku linaweza kutokea jambo baya lakini si sasa, huhitaji kuwa na hali ya hofu na kujipa matarajio ya jambo ambalo halipo kwa sasa,” alieleza mwanafamilia mmoja.
Wakati huo huo, kocha msaidizi wa timu ya Brazil, Cesar Sampaio ametaka kila mtu amuombee Pele baada ya chanzo kimoja cha habari nchini Brazil kudai kwamba nyota huyo wa zamani aliyebeba Kombe la Dunia mara tatu na timu ya Brazil ana hali mbaya.
“Bila kujali wewe ni wa dini gani tunaomba umuombee, ni mtu ambaye amenishawishi mimi si tu katika uanamichezo bali na ubinadamu pia,” alisema Sampaio ambaye kama Pele naye aliwahi kuwa mchezaji wa klabu maarufu nchini Brazil ya Santos.
Naye kocha wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger amesema kwamba Pele ni shujaa wake wa utotoni na anamuombea apone haraka.
Kimataifa Pele akutwa na korona
Pele akutwa na korona
Read also