Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba Queens, Charles Lukula ameeleza kuwa sare ya bao 1-1 waliyoipata dhidi ya Yanga Princess imetokana na kukosa umakini na kuzidiwa kipindi cha pili na wapinzani wao hao.
Timu hizo zinazoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake zilitoshana nguvu kwenye mchezo huo uliopigwa jana Jumatano kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Lukula alisema kulikuwa na nafasi kubwa ya kuondoka na pointi zote tatu lakini kwa kuwa mpira ni mchezo wa makosa, wanakubaliana na matokeo hayo na sasa wanajipanga kwa ajili ya kupata ushindi kwenye mchezo wao unaofuata dhidi ya Fountain Gate.
“Mpira ulikuwa mzuri, tulikuwa na nafasi ya kuchukua alama tatu lakini tumepoteza, mpira ni mchezo wa makosa, hivyo sasa tunaenda kujiandaa tuone kama tunaweza kupata matokeo kwenye mchezo unaofuata,” alisema.
“Lakini nawashukuru wachezaji walijituma ingawa goli moja huwezi kushinda mechi, nafikiri tungeongeza jingine ingekuwa sawa maana kipindi cha pili Princess walicheza vizuri kama ilivyokuwa kwetu kipindi cha kwanza, mwisho tukagawana pointi,” alisema Lukula.
Naye kocha msaidizi wa Princess, Fred Mbuna alisema: “Mechi imeisha salama, tumepata sare na sasa tunakwenda kujipanga kwa mchezo mwingine huu umeshapita, pointi moja hatukuitegemea kwenye mchezo huu lakini tunashukuru Mungu timu imeonesha kitu na imecheza vizuri.”
Kwa matokeo hayo, Simba iliyokuwa inaongoza msimamo wa ligi hiyo, sasa inashika nafasi ya tatu kwa pointi 27, Yanga ni ya nne kwa pointi 22 baada ya wote kucheza mechi 12. Fountain ipo kileleni kwa pointi 29 ikifuatiwa na JKT Queens yenye pointi 28.