Cairo, Misri
Hatma ya wapinzani wa timu za Simba na Yanga kwenye hatua ya robo fainali ya michuano ya klabu Afrika inatarajia kuwekwa hadharani kesho Jumatano na Shirikisho la Soka Afrika (Caf) katika droo itakayofanyika Cairo, Misri.
Droo hiyo inafanyika baada ya wikiendi iliyopita kukamilika kwa mechi za hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika inayoshiriki Simba na Kombe la Shirikisho Afrika inakoshiriki Yanga SC.
Upangwaji huo utakaofanyika saa 3.30 usiku kwa saa za Afrika Mashariki ikiwa ni saa 2.30 huko Misri, utafanyika kwa waliomaliza nafasi ya kwanza katika makundi kukutana na waliomaliza nafasi ya pili.
Simba iliyomaliza Kundi C nafasi ya pili ikiwa na pointi tisa nyuma ya vinara Raja Casablanca ya Morocco yenye pointi 16 inatarajia kupangwa na vigogo waliomaliza wa kwanza Kundi A, B na D.
Kinara wa Kundi A ni Waydad AC ya Morocco, Kundi B ni Mamelodi Sundowns na Kundi D ni Esperance ya Tunisia. Timu nyingine zilizomaliza nafasi ya pili ni Al Ahly ya Misri na CR Belouizdad na JS Kabylie zote za Algeria.
Yanga, wao walimaliza kinara wa Kundi D kwa pointi 13 sawa na US Monsatir ya Tunisia ambao ni mara ya kwanza kutinga robo fainali. Yanga iko juu kutokana na uwiano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Katika droo hiyo, Yanga inasubiri kupangwa na timu zilizokaa kwenye chungu cha waliomaliza nafasi za pili ambazo ni USM Alger ya Algeria kutoka Kundi A, Rivers United (Nigeria, Kundi B) na Pyramids (Misri, Kundi C).
Timu nyingine zilizomaliza vinara kwenye makundi yao kama Yanga ni Marumo Gallants ya Afrika Kusini, Asec Mimosas (Ivory Coast) na AS FAR (Morocco).
Kwa mujibu wa mashindano hayo, timu zinazomaliza nafasi ya kwanza kwenye makundi huwa na fursa ya kuanzia michezo yake ya hatua ya robo fainali ikiwa ugenini na kumalizia nyumbani.
Mechi za robo fainali Ligi ya Mabingwa zinatarajia kuanza kuunguruma Aprili 21 na kurudiana Aprili 28 wakati za Kombe la Shirikisho zikianza kutimua vumbi Aprili 23 na watarejeana Aprili 30, mwaka huu.
Kimataifa Wapinzani wa Simba, Yanga Caf hadharani
Wapinzani wa Simba, Yanga Caf hadharani
Read also
