Na mwandishi wetu
Nahodha msaidizi wa Azam FC, Sospeter Bajana amesema amejipanga kubeba tuzo ya mfungaji bora wa Ligi Kuu NBC msimu huu.
Akizungumza baada ya mchezo wao dhidi ya JKT Tanzania ambao walishinda kwa mabao 2-1 yeye akiwa mfungaji wa bao la kwanza, alisema pamoja na kucheza eneo la kiungo lakini amekuwa akijiongeza kwenda mbele kuwasaidia washambuliaji wao.
“Napenda sana kufunga na malengo yangu msimu huu ni kuwa mfungaji bora wa ligi kuu, naamini inawezekana kutokana na juhudi zangu ndani ya uwanja,” alisema Bajana.
Kiungo huyo mkabaji alisema anatambua haitokuwa kazi rahisi kutimiza lengo hilo kutokana na kuwepo washambuliaji wazuri kwenye timu yake na timu nyingine za Simba na Yanga lakini hilo halimpi presha ya kumfanya ashindwe kupambania malengo yake.
Alisema atahakikisha anapambana kupata nafasi ya kucheza kwenye kikosi chake cha Azam na kisha kupigania kutimiza ndoto yake ya ufungaji bora.
Bajana anayeshika nafasi ya tatu kwa ufungaji ndani ya kikosi cha Azam akiwa amefunga mabao matatu, winga Kipre Junior akifunga matano huku kiungo Feisal Salum ‘Fei Toto’ akiwa kinara wa timu hiyo kwa mabao yake saba.
