Na mwandishi wetu
Mshambuliaji wa Mashujaa, Reliant Lusajo ametamba kuifungia timu hiyo mabao ya kutosha kuliko alivyokuwa Namungo FC.
Akizungumza na GreenSports, mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga alisema anaamini atalitimiza hilo kutokana na uwepo wa viungo wenye uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi.
“Kazi yangu ni kufunga na ninaamini nitafunga mabao mengi sana sababu tuna viungo wenye uwezo wa kutoa pasi za mwisho na kufunga lakini pia nafasi ambayo kocha ananipanga inanipa urahisi wa kufanya hivyo,” alisema Lusajo.
Mchezaji huyo alisema mbali na uwepo wa viungo wengi wa kutengeneza nafasi lakini ana ushirikiano mzuri na mshambuliaji mwenzake Adam Adam hivyo hilo ni moja ya jambo ambalo linampa nguvu ya kuendeleza kile alichokifanya akiwa Namungo.
Alisema lengo lao yeye na mwenzake ni kuipigania timu hiyo kuondoka nafasi mbaya iliyopo hivi sasa na kukaa nafasi za juu ili kuendelea kushiriki Ligi Kuu NBC msimu ujao.
Lusajo aliyejiunga na timu hiyo kwenye dirisha dogo msimu huu, tayari ameifungia Mashujaa yenye maskani yake Kigoma mabao mawili katika michezo minne iliyopita.
Soka Lusajo kutupia mabao ya kutosha Mashujaa
Lusajo kutupia mabao ya kutosha Mashujaa
Read also