Na mwandishi wetu
Klabu ya Simba imetangaza kuwa itavaana mabingwa wa Zambia, Power Dynamos ya Zambia katika hitimisho la Wiki ya Simba, Simba Day Agosti 6, mwaka huu.
Kwa mujibu wa droo iliyofanyika leo Jumanne ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Simba huenda ikakutana na timu hiyo katika michuano hiyo kama timu hiyo ya Zambia itafanikiwa kusonga mbele.
Meneja Habari na Mawasiliano Simba, Ahmed Ally (pichani) akizungumza leo Jumanne jijini Dar es Salaam alieleza kuwa Wiki ya Simba itazinduliwa Julai 29, mwaka huu kwa kuchangia damu, kufanya shughuli za kijamii ikiwemo siku maalum ya kutembelea mashujaa wa Simba pia.
“Unyama mwingi ni usajili mzuri, tamasha kubwa, tunataka kutimiza malengo ambayo tumejiwekea ya kuchukua mataji yote ya ndani na kufanya vizuri kimataifa pia hivyo lazima jambo hili pia liwe kubwa.
“Siku ya Simba Day tutacheza na bingwa kutoka Zambia, Power Dynamos. Huyu ndiye tutacheza naye kwenye kilele cha Simba Week na kwa upande wa wasanii watoto wa nyumbani, Tunda Man, Meja Kunta na Whozu watakuwepo. Siku zinapokwenda tutaendelea kutangaza wasanii wengine ambao watakuwepo,” alisema Ally.
Tamasha hilo la Simba Day ambalo linafanyika kwa mara ya 14, ni maalum kwa ajili ya kutambulisha kikosi kipya cha timu hiyo kwa mashabiki tayari kuelekea kwenye mapambano ya msimu ujao.