Na mwandishi wetu
Timu ya Singida Fountain Gate imeuchagua Uwanja wa Black Rhino Academy uliopo Karatu, Arusha kwa ajili ya michezo zake za nyumbani.
Hiyo ni baada ya hivi karibuni Kamati ya Leseni za Klabu ya TFF kuufungia Uwanja wa Liti, Singida uliokuwa ukitumiwa na timu hiyo baada ya kubainika kuwa uwanja huo hauna sifa zinazohitajika.
Ofisa Habari wa Singida, Hussein Masanza (pichani juu) amesema leo Jumatano kuwa wameamua kuuchagua uwanja huo kutokana na ubora wake.
“Michezo yetu ya nyumbani sasa tutaenda kucheza kwenye Uwanja wa Black Rhino Academy hadi pale tutakaporuhusiwa tena kurudi nyumbani kutumia dimba la Liti.
“Kwa maana hiyo mchezo wetu dhidi ya KMC utakaochezwa Desemba 11, utapigwa Black Rhino, Karatu na maandalizi ya mechi hii yanaendelea vizuri, kikosi kinaendelea kujifua,” alisema Masanza.
Alisema wanaupa uzito mchezo huo kutokana na umuhimu wake kwani wametoka kudondosha pointi mbili dhidi ya JKT Tanzania hivyo wana kazi ya ziada kuhakikisha wanarudi kwenye njia yao ya ushindi.
Singida FG inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC ikiwa na pointi 19 baada ya kushuka uwanjani mara 12 ikishinda michezo mitano, sare nne na kupoteza mara tatu.