Na mwandishi wetu
Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB), Almasi Kasongo (pichani) amesema mafanikio ya klabu za Simba na Yanga kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika yametokana na uwekezaji mzuri uliofanywa na timu hizo.
Miamba hiyo ya soka nchini ni miongoni mwa timu nane Afrika zilizotinga robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kufanya vizuri kwenye mechi za hatua ya makundi.
Mtendaji huyo ameieleza GreenSports Jumanne hii kuwa uwekezaji uliofanywa na timu hizo mbili ndio msingi mkubwa wa mafanikio ya timu hizo, jambo ambalo timu nyingine zinapaswa kuiga mfano huo.
“Tunajivunia mafanikio ya Simba na Yanga, wameendelea kulitangaza soka la Tanzania lakini hiyo imetokana na uwekezaji na uaminifu wa viongozi wao ambao umeyashawishi makampuni kujitokeza kuwekeza wakiamini watapata faida,” alisema Kasongo.
Kiongozi huyo alisema mbali na hilo lakini kufanya vizuri kwa timu hizo kumethibitisha maana halisi ya kazi wanayoifanya ya kuongoza mpira wa miguu nchini pamoja na kuweka taratibu na sheria na kanuni zinazouendesha mchezo huo pendwa duniani.
Kasongo amezitaka klabu nyingine kuwa na njaa ya mafanikio kama ilivyo Simba na Yanga ili kupambana na kupata nafasi ya kushiriki mashindano hayo ya kimataifa ambayo ndani yake yana faida lukuki.
