New York, Marekani
Kocha na mchezaji wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani, Jurgen Klinsmann amesikitishwa na kitendo cha timu ya taifa hilo kutolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia 2026.
Ujerumani chini ya kocha Julian Nagelsmann imeziaga fainali hizo kwa kuchapwa mabao 4-3 na Paraguay katika mikwaju ya penalti baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya hatua ya 32 bora.
Klinsmann ambaye ameichezea timu ya taifa ya Ujerumani mara 108 kabla ya kuwa kocha wa timu hiyo na kuiongoza katika fainali za Kombe la Dunia 2006 ambapo ilimaliza nafasi ya tatu.
Akizungumzia kutolewa huko, Klinsmann alihoji maandalizi ya timu hiyo yalivyokuwa kabla ya mechi yao dhidi ya Paraguay iliyochezwa Jumatatu, Juni 28, 2026
“Ni wazi kwamba ni siku ya huzuni kwetu sote Wajerumani kwa sababu hatukutarajia kutolewa katika hatua ya pili (timu 32) na namna ambavyo tumetolewa ni jambo linalokatisha tamaa kwa kiasi kikubwa,” alisema Klinsmann.
Klinsmann alisema inaonekana timu haikujiandaa kukabiliana na hali ile ya kucheza kwa dakika 120 kwani wachezaji hawakuwa na nguvu kiasi cha kutosha na walikosa upambanaji dhidi ya timu imara ya Paraguay.
Hii inakuwa mara ya kwanza kwa Ujerumani kupoteza mechi ya fainali za Kombe la Dunia kwa penalti baada ya kushinda zote zilizopita kuanzia mwaka 1982 dhidi ya Ufaransa katika hatua ya nusu fainali.
Ujerumani pia ilizishinda timu za Mexico katika robo fainali mwaka 1986, England nusu fainali mwaka 1990 na Argentina robo fainali mwaka 2006.
