London, England
Vita ya Bayern Munich na PSG kuisaka saini ya straika wa Tottenham Hotspur, Harry Kane imechukua sura mpya baada ya straika huyo kudaiwa kusema kwamba yuko tayari kujiunga na Bayern na si PSG.
Kauli hiyo ya Kane inazidi kuifungulia njia Bayern kumpata Kane ambaye tayari amenukuliwa akisema kwamba anataka kutafuta changamoto mpya nje ya Spurs.
Kikwazo pekee kilichobaki sasa ni mabosi wa Spurs na Bayern katika kufanya biashara kwani zipo habari kwamba Spurs japo wapo tayari kumuuza Kane lakini wanataka kupiga pesa ndefu.
PSG inadaiwa ipo tayari kutoa Euro 100 milioni kiasi ambacho kinaweza kuongezeka kama straika wao tegemeo, Kylian Mbappe ataihama timu hiyo na kujiunga na Real Madrid kwa pesa ndefu.
Wakati PSG wakidaiwa kujiandaa kutoa pesa hizo, Spurs imeshakataa ofa mbili za Bayern, ya mwisho ni ya Euro milioni 90 ingawa klabu hiyo ya nchini Ujerumani bado haijakata tamaa ya kumpata Kane.
PSG pia inadaiwa kuendelea mazungumzo yao na kaka wa Kane aitwaye Charlie ambaye pia ndiye wakala wa mchezaji huyo ili kuhakikisha nahodha huyo wa England anasajiliwa na timu hiyo kutoka jiji la Paris nchini Ufaransa.
PSG pia inatambua utata uliopo katika kuipata saini ya Kane na tayari imeanza kuwafuatilia kwa karibu washambuliaji, Victor Osimhen wa Napoli ya Italia na Randal Kolo Muani wa Frankfurt ya Ujerumani.
Katika hatua nyingine, kocha mpya wa Spurs, Ange Postecoglou amenukuliwa akisema kwamba amefanya mazungumzo na Kane kuhusu mechi ya kujiandaa na msimu mpya dhidi ya West Ham.
“Nimekuwa na mazungumzo mazuri na Harry, si mambo ya kushtua kama watu wanavyotegemea, ni mazungumzo mazuri tu, nimejitambulisha na tumezungumza zaidi kuhusu klabu na wapi anadhani kunahitaji maboresho,” alisema Postecoglou.
Kimataifa Kane aikataa PSG, aitaka Bayern
Kane aikataa PSG, aitaka Bayern
Read also
