Riyadh, Saudi Arabia
Mshambuliaji wa Brazil, Neymar amesema kwamba alipitia kupindi kigumu yeye na mshambuliaji mwenzake Lionel Messi wakati wakiichezea klabu ya Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa.
Neymar na Messi wote waliihama PSG katika majira ya kiangazi msimu huu, Neymar akijiunga na klabu ya Al Hilal ya Saudi Arabia kwa ada ya Dola 98.6 milioni wakati messi alijiunga na Inter Miami ya Marekani akiwa mchezaji huru.
Kauli hiyo ya Neymar imekuja baada ya mchezaji huyo kuulizwa kuhusu Messi kubeba Kombe la Dunia na timu ya Argentina ambapo alisema alifurahi mwenzake alipobeba taji hilo la dunia lakini alikuwa na huzuni kwa kilichokuwa kikiendelea PSG.
“Nilikuwa mwenye furaha kwa jinsi mwaka wake ulivyokuwa lakini pia nilikuwa na huzuni kwa sababu alikuwa na upande mwingine, alikuwa mwenye furaha akiwa na Argentina akishinda mataji mengi na kwa PSG ilikuwa majanga kwake na kwangu,” alisema Neymar.
Messi na Neymar waliwahi kucheza pamoja Barcelona na kushinda mataji ya Ligi I Ufaransa lakini katika klabu hiyo walishindwa kubeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Messi ambaye naye alikuwa na wakati mgumu PSG aliwahi kunukuliwa akisema kwamba kwa misimu miwili aliyoichezea timu hiyo, kulikuwa na tatizo kati yake na baadhi ya mashabiki.
Neymar na Messi waliwahi kukutana na matukio ya kuzomewa na mashabiki wa PSG katika miaka yao miwili baada ya timu hiyo kutolewa kwenye fainali za Ligi ya Mabingwa Ulaya.