Na mwandishi wetu
Sakata la klabu ya Yanga na kiungo wake, Feisal Salum au Fei Toto huenda likafika mwisho baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaomba viongozi wa klabu hiyo kumaliza mzozo wao na mchezaji huyo.
Rais Samia ametoa kauli hiyo Ikulu leo Jumatatu wakati wa hafla ya chakula cha jioni aliyowaandalia wachezaji na viongozi wa Yanga kuwapongeza kwa kufikia hatua ya fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Yanga imeingia katika mzozo na mchezaji huyo tangu Desemba mwaka jana alipowasilisha maombi ya kutaka kuvunjiwa mkataba lakini uongozi wa Yanga haukukubaliana naye na hadi sasa mzozo huo unaendelea.
Baada ya Yanga kukataa kuvunja mkataba, Fei aliamua kwenda kuishitaki klabu hiyo TFF lakini kamati husika ya TFF haikukubaliana na hoja zake na kwa sasa zipo habari kwamba ana mpango wa kulifikisha suala hilo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Michezo (CAS).
Hivi karibuni Rais wa Yanga, Hersi Said alizungumza na kituo kimoja cha redio na kusema kwamba hawana tatizo na Fei na kumtaka arudi kuitumikia Yanga na kama kuna klabu inayomtaka ijitokeze.
Kwa upande wake Fei ameendelea kusisitiza nia ya kutaka kuihama Yanga akidai kwamba amekuwa akinyanyaswa na hata kutuhumiwa kuuza mechi na aliwahi kufanya mazungumzo na Hersi kwa saa sita lakini hawakufikia muafaka.
Wakati Hersi akimtaka Fei arudi Yanga, mchezaji huyo alinukuliwa akisema kwamba atakuwa tayari kurudi katika klabu hiyo iwapo tu Hersi ataondoka.
Katika hoja yake ya kutaka sakata la Fei Toto na Yanga limalizwe Rais Samia alisema haipendezi kwa klabu hiyo kubwa kama ya Yanga kuwa na ugomvi na Fei Toto.
“Viongozi wa Yanga nina ombi kwenu, sifurahii kusikia mnakuwa na mizozo na wachezaji, na sitaki kusema mengi nataka niwaambie tu ishu ya Fei Toto hebu kaimalizeni, kaimalizeni ili tuangalie mbele,” alisema Rais Samia.
Rais Samia alisema haipendezi klabu kubwa kama ya Yanga iliyofanya kazi nzuri inakuwa na ugomvi na katoto na angependa kupewa mrejesho wa hilo na akawakaribisha viongozi kumpa mrejesho wa suala hilo siku yoyote wakiwa tayari.