London, England
Ushindi wa bao 1-0 ambao imeupata Arsenal katika mechi ya Ligi Kuu England dhidi ya Newcastle umekuwa na furaha kubwa kwa kocha wa timu hiyo Mikel Arteta katika mbio za kulisaka taji la ligi hiyo msimu huu.
Arsenal ilipata pigo baada ya kupoteza mechi yake dhidi ya Man City, matokeo yaliyoacha dalili mbaya katika mbio hizo lakini ushindi dhidi ya Newcastle umempa faraja kocha huyo ambaye sasa timu yake ipo kileleni ikiwa imeizidi Man City kwa pointi tatu.
Bao hilo pekee lililompa furaha Arteta lilifungwa na Eberechi Eze limetosha kuifanya Arsenal ipate nguvu mpya ya kuendeleza mapambano siku chache zikiwa zimepita baada ya kipigo cha mabao 2-1 mbele ya Man City.
“Kwa hakika nina furaha kwa kupata ushindi, tulizungumza kuhusu hii mechi moja na kwa kiasi gani ilikuwa yenye umuhimu, tuliifanya kazi, tulilazimika kufanya kile tulichokiweza na tulilijadili hilo,” alisema Arteta.
Ushindi ambao Man City iliupata katikati ya wiki dhidi ya Burnley ulimaanisha kwamba Arsenal ilishuka hadi nafasi ya pili ikiwa ni mara ya kwanza tangu Oktoba mwaka jana baada ya timu kuwa sawa kwa pointi na Man City ambayo ilishika usukani kutokana na wingi wa mabao ya kufunga.
Mazingira hayo yaliiweka katika hali ngumu Arsenal na hivyo mechi yao na Newcastle ilikuwa hatua muhimu ya mapambano yao ya kulisaka taji la ligi hiyo na ushindi umekuwa na maana kubwa kwa timu hiyo.
Hali ya furaha kwa kupata ushindi dhidi ya Newcastle ilijidhihirisha baada ya wachezaji kulala chini pale mwamuzi alipopuliza filimbi kuashiria kumalizika kwa mchezo huo.
Kuhusu mechi nne zilizobaki kabla ya ligi kufikia tamati, Arteta alisema yuko tayari kukabiliana na hali ya presha ya mapambano ili kumaliza ukame wa taji la ligi hiyo ambalo wamekuwa wakilisubiri kwa miaka mingi sasa.
