Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ ameuagiza uongozi wa Simba kusajili wachezaji watano wenye ubora wa hali ya juu ili timu hiyo iweze kugombania mataji katika michuano yote watakayoshiriki msimu ujao.
Simba ambayo inaelekea kumaliza msimu wa pili bila kubeba taji lolote ndani na nje ya Tanzania, inahitaji kufanya usajili huo ili kuboresha kikosi chake ambacho kwa mujibu wa kocha huyo raia wa Brazil kimeshindwa kupambana kutokana na kukosa wachezaji bora.
Robertinho amezitaja nafasi ambazo anahitaji kuziboresha kuwa ni mshambuliaji, kiungo mkabaji, beki wa kati, winga na beki wa pembeni mmoja ili waweze kuwa washindani wa kweli hasa kwenye mashindano ya kimataifa.
“Kilichotukwamisha msimu huu ni mapungufu yaliyopo ndani ya kikosi chetu, tulikosa wachezaji wenye sifa ya upambanaji hasa kwenye michuano ya kimataifa, hili nitaliweka hata kwenye ripoti yangu baada ya msimu kumalizika,” alisema Robertinho.
Kocha huyo ameeleza kuwa mpira wa siku hizi unachezwa kimbinu zaidi na hiyo inategemea na aina ya wachezaji waliopo kwenye kikosi, kukosekana kwa wachezaji wenye viwango kama anaowahitaji ndio kulichangia safari yao iishie njiani.
Robertinho alisema katika hilo hawezi kumtupia lawama mchezaji yeyote sababu waliopo walipambana kadri ya uwezo wao mpaka hapo walipofika na kwake wanastahili pongezi kutokana na kucheza kwa kujitoa katika mashindano yote msimu huu.
Mbrazili huyo ameutaka uongozi wa timu hiyo kukamilisha jambo hilo mapema ili kupata muda wa kuiandaa timu hiyo kabla ya kuanza kwa michuano ya Caf Super League mwezi Agosti, mwaka huu.
Mpaka sasa zikiwa zimesalia mechi tatu kabla ya kumalizika Ligi Kuu NBC, Simba inashikilia nafasi ya pili kwa pointi 64 nyuma ya vinara Yanga wenye pointi 71.
Pia Wekundu hao Jumapili iliyopita walifungwa mabao 2-1 na Azam FC kwenye nusu fainali ya Kombe la FA (ASFC) na kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika pia wametupwa nje baada ya kufungwa kwa matuta 4-3 na Wydad Casablanca ya Morocco katika hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.