Na mwandishi wetu
Kocha Mkuu wa Simba, Roberto Oliviera ‘Robertinho’ ameanza kujiwinda na mechi dhidi ya mahasimu wao Yanga maarufu Dar Derby akisema ataitumia mechi dhidi ya Ihefu FC kujiandaa na mechi hiyo.
Yanga na Simba zitaumana Aprili 16 mwaka huu kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam ingawa kabla ya mechi hiyo, Simba watakuwa wenyeji wa Ihefu FC wikiendi hii katika mechi ya robo fainali ya Kombe la FA (ASFC) itakayopigwa kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Robertihno alisema maandalizi ya mchezo na Ihefu yamekamilika na wachezaji wako kwenye hali nzuri, anaamini wataenda kupata ushindi na kusonga mbele japo anaiheshimu Ihefu kutokana na ubora wa kikosi chao.
“Malengo yetu ni kuhakikisha tunashinda michezo yote iliyo mbele yetu ili kuweka hai matumaini ya kushinda makombe yaliyo mbele yetu ya ndani na Ligi ya Mabingwa Afrika.
“Natambua ugumu wa mechi zilizopo mbele yetu, tunahitaji ushindi katika mchezo dhidi ya Ihefu ili kujiweka sawa dhidi ya Yanga, ni michezo miwili ambayo nina imani itakuwa migumu kutokana na ubora wa wapinzani wetu.
“Napenda sana michezo ya Derby, ndiyo kipimo kizuri tunahitaji ushindi kwenye mechi hii ili kupunguza idadi ya pointi baina yetu na wao jambo zuri ni kuwa kikosi changu kimeendelea kuimarika wachezaji waliokuwa na majeruhi wameanza kurejea hivyo nitakuwa na wigo mpana wa kikosi,” alisema Robertinho.
Yanga ipo kileleni kwa pointi 65 dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili kwa pointi 57 baada ya wote kucheza mechi 24 mpaka sasa, zikiwa zimesalia mechi sita kabla ya ligi kumalizika.
Soka Robertinho aanza hesabu za Dar Derby
Robertinho aanza hesabu za Dar Derby
Read also