Na mwandshi wetu
Bondia wa Tanzania, Abdallah Abdallah ‘Katoto’ amevunjika mkono kwenye raundi ya mwisho ya pambano lake dhidi ya bondia wa Ethiopia, Wibshet Bekele katika michezo ya Afrika inayoendelea nchini Ghana.
Kwa mujibu wa Rais wa Shirikisho la Ngumi Tanzania (BFT), Lukelo Willilo, Katoto alipata ajali hiyo akijiandaa kufanya shambulizi dhidi ya mpinzani wake raundi ya tatu na ya mwisho ya mchezo huo wa hatua ya 16 bora uliochezwa jana Ijumaa.
“Mwamuzi alilazimika kusimamisha pambano, Katoto tulimuwahisha kwenda University of Ghana Medical Center kwa ajili ya matibabu; na baada ya kuchukuliwa vipimo alionekana amevunjika sehemu ya katikati ya mkono.
“Ila tunashukuru Mungu hali yake inaendelea vizuri ingawa hataweza kucheza kwa kipindi cha karibuni,” alisema kocha msaidizi wa timu ya taifa ya ngumi, Muhsini Mng’ola.
Baada ya pambano hilo, Katoto alikuwa apambane hatua ya robo fainali dhidi ya Patrick Chinyemba kutoka Zambia ambaye ni Bingwa wa Afrika na tayari ameshakata tiketi ya kufuzu kushiriki Olimpiki ya Paris 2024.
“Ndoto yangu kubwa ilikuwa katika pambano langu la robo fainali dhidi ya Chinyemba wa Zambia na kutaka kuishangaza Afrika na dunia kwa uwezo wangu, pambano hili la Muethiopia nilikuwa nina uhakika na ushindi kwa maandalizi mazuri tuliyoyapata,” alisema Katoto.
Kwa upande wake Willilo alisema: “Tunamshukuru Mungu kwa yote, ndio mchezo ulivyo, zilikuwa zimebaki sekunde chache pambano liishe huku tukiongoza kwa matokeo, lakini mchezo wakati mwingine una matokeo katili.”