Na mwandishi wetu
Aliyekuwa Mbunge wa Tabora Mjini, Ismail Rage, ameupongeza uongozi wa timu ya Tabora United kwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kucheza soka la ushindani.
Rage ambaye pia aliwahi kuwa Mwenyekiti wa klabu ya Simba na katibu mkuu wa TFF (enzi za FAT) alisema kiwango na matokeo ambayo timu hiyo imeyapata katika mechi tano za ligi walizocheza yanadhihirisha namna walivyojipanga kutoa upinzani msimu huu.
“Nawapongeza viongozi wa Tabora United, wametengeneza timu nzuri na benchi la ufundi imara sana kwa matokeo na nafasi waliyopo kwenye msimamo katika mechi tano walizocheza inaonesha wamekuja kushindana siyo kuzisindikiza Simba na Yanga,” alisema Rage.
Kiongozi huyo alisema ameshuhudia mechi mbili za timu hiyo wakiwa nyumbani Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi ameona namna wachezaji na Kocha Mkuu, Goran Kopunovic wanavyojituma kutafuta ushindi kitu ambacho hakipatikani kwa baadhi ya timu kubwa nchini.
Alisema kwa ari ya upambanaji waliyonayo Tabora, timu nyingi zikiwemo Simba na Yanga zijipange ikiwemo kujiandaa kupoteza mchezo.
Rage alisema kama timu hiyo itaendelea hivyo anaamini kuna uwezekano ikamaliza nafasi nne za juu na mwakani ikawakilisha taifa kwenye michuano ya kimataifa.
Tabora United inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa Ligi Kuu NBC ikiwa na pointi nane katika mechi tano walizocheza hadi sasa.