Na mwandishi wetu
Rais wa timu ya Singida Fountain Gate, Japhet Makau amesema baada ya kushindwa kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, sasa malengo yao ni kutwaa Kombe la FA (ASFC) na kumaliza nafasi tatu za juu kwenye Ligi Kuu NBC.
Singida FG Licha ya kutolewa kwenye Kombe la Shirikisho, timu hiyo pia imeanza ligi kwa kusuasua baada ya kupata sare mbili na kupoteza mchezo mmoja kwenye michezo mitatu waliyoshuka dimbani mpaka sasa.
“Tukiachana na ligi lakini lengo letu lingine ni kufanya vizuri katika Kombe la FA, hapa tunahitaji kutwaa taji la michuano hiyo ili kurejea kwa mara ya pili kushiriki michuano ya kimataifa.
“Ni kweli tulikutana na sintofahamu za makocha wetu akiwemo Ernest Middendorp kuondoka, hiyo changamoto imetokea kwenye timu, na sasa tuko kwenye hatua za mwisho kumalizana na kocha wetu mpya,” alisema Makau.
Aliongeza kuwa baada ya mechi yao ya kesho dhidi ya Mtibwa Sugar watakuwa wamekamilisha mchakato wa kupata kocha mkuu, wakitarajia uwepo wake kwenye mechi yao dhidi ya Simba, Oktoba 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Liti, Singida.
