New Jersey, Marekani
Mshambuliaji nyota wa Brazil, Neymar Jr ametangaza rasmi kuachana na timu yake ya taifa baada ya kutolewa na Norway katika hatua ya 16 bora ya fainali za Kombe la Dunia 2026.
Brazil maarufu Selecao imeziaga rasmi fainali hizo kwa kipigo cha mabao 2-1 mbele ya Norway, mechi iliyopigwa Jumatatu, Julai 6, 2026 kwenye Uwanja wa MetLife mjini New Jersey.
Aliyepeleka msiba Brazil na kusababisha Neymar atangaze kuachana na timu yake ya taifa si mwingine bali ni mshambuliaji nyota wa Man City, Erling Haaland aliyefunga mabao hayo mawili katika dakika za 79 na 90.
Haaland pia aliibuka shujaa katika mpambano wake uliozoeleka na Gabriel, beki wa Brazil na timu ya Arsenal na mashabiki kuwatolea macho kwa namna ambavyo wamekuwa wakichuana katika klabu zao hasa kwenye Ligi Kuu England na hatimaye kwenye timu za taifa.
Katika mechi hiyo Neymar, 34, aliingia uwanjani dakika ya 67 lakini uwepo wake haukuweza kuisaidia timu hiyo kutoka uwanjani na ushindi na mwisho wake alitoka uwanjani akilia.
Kitu pekee alichofanya Neymar uwanjani ni kufunga bao la mkwaju wa penalti dakika za nyongeza, bao lililoishia kuwa faraja kwa timu hiyo na mchezaji huyo ambaye kwa kauli yake hiyo inakuwa mechi yake ya mwisho.
“Nimejitahidi na kujitahidi lakini sasa nimefika mwisho, nilianzia hapa na nimemalizia hapa,” alisema Neymar huku akitokwa machozi.
Kauli ya Neymar inakumbushia mwanzo wake na timu ya Brazil, alipoichezea mara ya kwanza Agosti 2010 kwenye uwanja huo huo katika mechi ya kirafiki dhidi ya Marekani na kufunga bao katika ushindi wa 2-0.
Tangu wakati huo hadi sasa Neymar amepiga hatua kwa kuweka rekodi ya kipekee akiifungia timu ya Brazil mabao 80 na kuwa mchezaji anayeongoza kwa kuifungia timu hiyo mabao mengi.
Zaidi ya hilo, Neymar pia anashika nafasi ya pili kwa kuichezea Brazil mechi 130 akiwa ametanguliwa na beki wa zamani wa timu hiyo, Cafu ambaye ameichezea Brazil mara 142.
Hizi ni fainali za nne za Kombe la Dunia kwa Neymar ambaye alipewa nafasi kubwa ya kuibeba timu hiyo katika fainali hizi zilizotabiriwa kuwa za mwisho kwake baada ya kuiwakilisha katika fainali za 2014, 2018 na 2022.
